ALHAMISI JUMA 31 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Flp.3:3-8
Sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumaini mwili. Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu yeyote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:2-7(K)3
1. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.

(K) Ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.

2. Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake siku zote.
Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya,
Miujiza yake na hukumu za kinywa chake. (K)

3. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake,
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye Bwana, ndiye Mungu wetu,
Duniani mwote mna hukumu zake. (K)

SHANGILIO: Yn.10:27
Aleluya, aleluya!
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya!

INJILI: Lk.15:1-10
Watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia Yesu wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao. Akawaambia mfano huu, akisema, Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aenda akamtafute yule aliyepotea hata amwone? Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi. Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea. Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu. Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione? Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea. Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.