ALHAMISI JUMA 33 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Ufu.5:1-10
Mimi, Yohane, niliona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na nyumba, kimetiwa muhuri saba. Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, N’nani astahiliye kukifungua kitabu, na kuzivunja muhuri zake? Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba. Nikaona katikati ya kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwanakondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote. Akaja, akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi. Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwanakondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu. Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.149:1-6,9
Aleluya.
1. Mwimbieni Bwana mwimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfuhie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.

(K) Ulitufanya kuwa wafalme na makuhani.

2. Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)

3. Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote.
Aleluya. (K)

SHANGILIO: Yn.17:17
Aleluya, aleluya!
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya!

INJILI: Lk.19:41-44
Yesu alipofika karibu ya Yerusalemu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe, katika siku hii, yapasayo Amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu Wapendwa, katika siku yake Yerusalemu hakuyajua yapasayo amani. Kwa vile sisi tunahitaji neema ya Mungu, tuombe.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Viongozi wetu wa Kanisa wazidi kuhubiri amani na ulinzi wa imani yetu ya kweli. Ee Bwana.

2. Wote wenye mamlaka serikalini wajaliwe busara na utu wema, wapate kutatua kwa njia za haki na amani migogoro yote inayowakera raia wao. Ee Bwana.

3. Utujalie kuzishika kiaminifu mila njema za wazee wetu, tupate kuiiga imani yao kwako na kuitetea mpaka mwisho. Ee Bwana.

4. Ekaristi Takatifu ituimarishe katika kumjua na kumpenda Kristo Mwanao, aliyechinjwa sadaka kwa ajili ya watu wa dunia nzima; na akawafanya kuwa ufalme na makuhani kwako. Ee Bwana.

5. Marehemu wanaongojea huruma yako waipate na kukaribishwa kwako mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetaka tukupende Wewe zaidi ya chochote uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu Amina.