ALHAMISI JUMA 3 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.10:19-25
Ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya,
iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu; na
tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya,
tumeoshwa miili kwa maji safi. Na mlishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi
ni mwaminifu; tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache
kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri
mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.24:1-6 (K)6
1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
(K) Hiki ndicho kizazi cha waufuatao uso wako, Ee Bwana.
2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K)
3. Atapokea baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)
SHANGILIO: 1Pet.1:25
Aleluya, aleluya!
neno la Bwana hudumu milele.”
Neno hilo ni hiyo Habari Njema mliyohubiriwa.
Aleluya!
INJILI: Mk.4:21-25
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa
juu ya kiango? Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna
lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.
Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.
Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tumwombe Mungu kwa moyo mkunjufu na imani
timilifu tukisema:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umjalie Askofu wetu F. na makuhani wote moyo
thabiti na afya njema, wapate kupaingia patakatifu
pako na kuadhimisha Ekaristi Takatifu. Ee Bwana.
2. Viongozi wa serikali na wote wenye mamlaka wasisite
kuwaonya na kuwaelekeza wanaokiuka sheria halali
za nchi yetu. Ee Bwana.
3. Utupe moyo wa kuangaliana sisi kwa sisi kwa upendo,
na utujalie kuona uzuri wa kuumega mkate pamoja.
Ee Bwana.
4. Uzibariki nyumba na familia zetu; uwaite vijana
wengi kuingia miito mitakatifu na uwaimarishe
walioitikia miito hiyo katika kukutumikia kwa
moyo mnyofu. Ee Bwana.
5. Uwajalie marehemu wetu kusimama katika patakatifu
pako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Bwana Mungu, mwenye kitu atapewa zaidi. Uipokee
sala yetu sisi tukutafutao. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.