ALHAMISI JUMA 4 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Ebr.12:18-19, 21-24
Ndugu zangu hamkufikilia mlima uwezao kuguswa, uliowaka moto, wala wingu jeusi, na giza, na tufani, na mlio wa baragumu na sauti ya maneno; ambayo wale walioisikia walisihi wasiambiwe neno lo lote lingine; Na hayo yaliyoonekana jinsi yalivyokuwa ya kutisha, hata Musa akasema, Nimeshikwa na hofu na kutetemeka. Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.48:1-3,8-10. (K)9
1. Bwana ndiye aliye mkuu,
Na mwenye kusifiwa sana.
Katika mji wa Mungu wetu,
Katika mlima wake mtakatifu.
Kuinuka kwake ni kuzuri sana,
Ni furaha ya dunia yote.

(K) Tumezitafakari fadhili zako,
Ee Mungu, katikati ya hekalu lako.

2. Mlima Sayuni pande za kaskazini,
Mji wa Mfalme mkuu.
Mungu katika majumba yake
Amejijulisha kuwa ngome. (K)

3. Kama tulivyosikia, ndivyo tulivyoona,
Katika mji wa Bwana wa majeshi.
Mji wa Mungu wetu;
Mungu ataufanya imara hata milele. (K)

4. Tumezitafakari fadhili zako, Ee Mungu,
Katikati ya hekalu lako.
Kama lilivyo jina lako, Ee Mungu,
Ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia.
Mkono wako wa kuume umejaa haki; (K)

SHANGILIO: Zab.147:12,15
Aleluya, aleluya,
Umsifu Mwenyezi Mungu, ee Yerusalemu!
Umsifu Mungu wako, ee Siyoni!
Yeye hupeleka amri yake duniani,
na neno lake hufikia lengo lake haraka.
Aleluya.

INJILI: Mk.6:7-13
Yesu aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu; akasema, Msivae kanzu mbili. Akawaambia, Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale. Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung'uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao. Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu, Wewe unakuwa daima kati yetu kwa namna mbalimbali, hasa tunapoadhimisha Ekaristi Takatifu. Kwa imani tunakuomba:-

Kiitikio: Utupe neema yako.
1. Kanisa lako lizidi kuadhimisha mafumbo matakatifu ambayo kwayo twakutana nawe. Ee Bwana.

2. Maaskofu, Mapadre na Mashemasi wetu wazitunze vema neema walizozipokea kwa Sakramenti ya Daraja Takatifu. Ee Bwana.

3. Wabatizwa wote daima wapende kukutolea Wewe Mungu sadaka safi na yenye kupendeza mbele zako. Ee Bwana.

4. Utujalie sisi sote uhodari, tuyashike mausia yako, twende katika njia zako, tuzishike sheria na amri zako kwa moyo wote; tupate kufika kwako mbinguni. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wakwezwe mlimani Sayuni, mpaka kwenye mji wako Mungu uliye hai. Ee Bwana.

Ee Bwana Mungu unayetualika kuitikia kila siku wito wako wa kuihubiri Habari njema, utujalie hayo yote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.