ALHAMISI JUMA 6 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Mwa.9:1–13
Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi. Kila mnyama wa katika nchi atawaogopa ninyi na kuwahofu, na kila ndege wa angani; pamoja na vitu vyote vilivyojaa katika ardhi, na samaki wote wa baharini; vimetiwa mikononi mwenu. Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu, kama nilivyowapa mboga za majani, kadhalika nawapeni hivi vyote. Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile. Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu. Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na wanadamu; maana kwa mkono wake Mungu alimfanya mwanadamu. Nanyi zaeni, mkaongezeke; zaeni sana katika nchi, mkaongezeke ndani yake. Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema, Mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi; tena na uzao wenu baada yenu; tena na kila kiumbe hai kilichopo pamoja nanyi, ndege, kila mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi. Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo kuiharibu nchi. Mungu akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.102:15–20,28,21–22 (K)19
1. Mataifa wataliogopa jina la Bwana.
Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
Atakapoonekana katika utukufu wake,
Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,
Asiyadharau maombi yao.

(K) Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi.

2. Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,
Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,
Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi
Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,
Na kuwafungua walioandikiwa kufa. (K)

3. Wana wa watumishi wako watakaa,
Na wazao wataimarishwa mbele zako.
Watu walitangaze jina la Bwana katika Sayuni,
Na sifa zake katika Yerusalemu.
Pindi mataifa watakapokusanyika pamoja,
Falme nazo ili kumtumikia Bwana. (K)

SHANGILIO: Zab.147:12,15
Aleluya, aleluya!
Msifu Bwana, ee Yerusalemu,
na neno lake nimelitumainia.
Aleluya!

INJILI: Mk.8:27–33
Siku ile Yesu alitoka na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria-Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, Watu huninena mimi kuwa ni nani? Wakamjibu, Yohane Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo. Akawaonya wasimwambie mtu habari zake. Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Hapo, Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea. Lakini Yesu akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, tumwombe Mungu aliyembariki Nuhu na kufanya naye agano. Ee Mungu twakuomba:-

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa wazidi kuishuhudia imani yao kwa Kristo na kumtambulisha kwa watu. Ee Bwana.

2. Hata watawala wa dunia wakukiri Wewe na Mwanao Yesu Kristo, ili ufalme wako uenee duniani kote. Ee Bwana.

3. Utuepushe na kishawishi cha ubaguzi wa aina yoyote, kwani umetufundisha kuwa maskini wa dunia hii ndio uliowachagua wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme uliowaahidia wakupendao. Ee Bwana.

4. Kwa adhimisho la Ekaristi Takatifu, utujalie kulishika kiaminifu agano jipya na la milele, uliloliweka nasi kwa kifungo cha upendo usio na kikomo. Ee Bwana.

5. Uwapokee marehemu wetu kwenye ufalme wako wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetujalia mema mengi wakati wa taabu na raha, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina