ALHAMISI JUMA 7 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO: YbS.5:1–8
Usizitumainie mali zako, wala usiseme, Zanitosha basi. Usifuate roho yako na nguvu zako, kuandamana
na tamaa za moyo wako. Usiseme, nani atakayenitawala? Hakika Bwana atakulipiza kisasi. Usiseme,
Nalikosa ikanipata nini? Hakika Bwana ndiye mvumilivu. Mintarafu upatanisho, usiwe mjasiri wa kutenda
dhambi juu ya dhambi; wala usiseme, Huruma zake zi nyingi. Kwa sababu rehema na ghadhabu zatoka kwake,
na hasira yake itawakalia wakosaji. Usichelewe kumrudia Bwana, wala usikawie siku kwa siku; kwa maana
ghadhabu ya Bwana itatokea kwa ghafula, nawe utaangamia wakati wa kisasi. Wala usizitegemee mali za
udhalimu, kwa kuwa hazitakufaidia lolote siku ile ya hasira.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.1:1–4,6 (K)Zab.40:4
1. Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
(K) heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.
2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)
3. Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)
SHANGILIO: Zab.119:105
Aleluya, aleluya!
Neno lako ni taa ya miguu yangu,
na mwanga wa njia yangu.
Aleluya!
INJILI: Mk.9:41-50
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Yeyote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi
ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake. Na yeyote atakayemkosesha mmojawapo
wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini.
Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono
miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.
Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete kuliko kuwa na miguu
miwili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Na jicho lako
likikukosesha, ling’oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa
na macho mawili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Kwa sababu
kila mtu atatiwa chumvi kwa moto. Chumvi ni njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena, mtaitia nini
ikolee? Mwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa Mungu ndiye mpaji wa vyote,na
mwenye rehema na haki, tumwombe katika shida zetu
na za Taifa lake kwa ujumla.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa
lako, wasichoke kuwahubiria watu toba hasa katika
maadhimisho ya Ekaristi Takatifu. Ee Bwana.
2. Mahakimu na wasuluhishi wa kesi za watu wajaliwe
kutoa hukumu za haki wakizingatia roho ya sheria.
Ee Bwana.
3. Kwa namna ya pekee utetee haki za wanyonge
dhidi ya wanaojinufaisha kwa tamaa na kufanya
anasa kinyume cha sheria na amri zako. Ee Bwana.
4. Kwa huruma na upendo wako, utuokoe na yule mwovu,
na utujalie msamaha wa dhambi zote. Ee Bwana.
5. Uwasamehe marehemu wetu ambao bado wanaihitaji
huruma yako. Ee Bwana.
Ee Mungu mwenye kuilinda kazi ya huruma yako ndani
yetu, utujalie hayo tuliyokuomba. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.