IJUMAA JUMA 1 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: Isa.29:17-24
Bwana Mungu asema: Je! Si muda mdogo uliobaki, na Lebanoni itageuzwa kuwa shamba lizaalo sana, na lile
shamba lizaalo sana litahesabiwa kuwa msitu? Na katika siku hiyo viziwi watasikia maneno ya hicho chuo,
na macho ya vipofu yataona katika upofu na katika giza. Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana,
na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli. Kwa maana mwenye kutisha ameangamizwa,
naye mwenye dharau amekoma, nao wote watazamiao uovu wamekatiliwa mbali; hao wamfanyao mtu kuwa amekosa
katika neno, na kumtegea mtego yeye aonyaye langoni, na kumgeuza mwenye haki kwa kitu kisichofaa. Basi,
Bwana aliyemkomboa Ibrahimu asema hivi, katika habari za nyumba ya Yakobo; Yakobo hatatahayarika sasa,
wala uso wake hautabadilika rangi yake. Basi atakapowaona watoto wake, walio kazi ya mikono yangu, katikati
yake, wao watalitakasa jina langu; naam, watamtakasa Mtakatifu wa Yakobo, nao watamcha Mungu wa Israeli.
Hao nao wakosao rohoni mwao watapata kufahamu, na hao wanung’unikao watajifunza elimu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.27:1,4,13-14
1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani? (K)
(K) Bwana ni nuru ya wokovu wangu.
2. Neno moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani kwa Bwana,
Siku zote za maisha yangu.
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake. (K)
3. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana,
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Tazama Bwana wetu atakuja na nguvu, Na atayaangaza macho ya watumishi wake.
Aleluya.
INJILI: Mt.9:27-31
Siku ile: Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu,
Mwana wa Daudi. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza
kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana. Ndipo alipowagusa macho yao yakafumbuka. Naye Yesu akawaagiza kwa
nguvu, akisema, Angalieni hata mtu mmoja asijue. Lakini wakatoka, wakaeneza habari zake katika nchi ile yote.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, ujio wa Kristo utaleta mapinduzi ya kiroho na kimwili, na wazao wa Yakobo watalitakasa jina la Bwana.
Kwa kuwa sisi ndio jamaa ya Yakobo, tuombe:
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Umjalie kila mmoja wetu kukumbuka kuwa muda uliobaki kwa ujio wa Bwana ni mdogo na kwamba siku ya
wokovu ndiyo sasa.
2. Utuongezee furaha na bidii katika kufanya mageuzi ya kiroho na kimwili kwa ajili ya ujio wa Mkombozi
wetu.
3. Utegue mitego ya yule adui mwovu, ili Mkombozi wetu ajapo tumpokee bila kizuizi chochote.
4. Uturehemu; na uyafumbue macho yetu tupate kuyaona yaliyo mema, ili tuweze kuendelea kuieneza Habari
Njema duniani kote.
Ee Mungu, Baba mwenye huruma na mapendo, Neno lako liguse daima mioyo yetu tukuongokee wewe. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.