IJUMAA JUMA 1 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.4:1-5,11
Ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana ni
kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao,
kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile;
kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu: Kwa maana ameinena siku ya
saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo, Hawataingia
rahani mwangu. Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa
mfano uo huo wa kuasi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.78:3-4,6-8 (K)7
1. Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu,
Ambayo baba zetu walituambia.
Huku tukiwaambia kizazi kingine,
Sifa za Bwana, na nguvu zake,
(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.
2. Ili kizazi kingine wawe na habari,
Ndio hao wana watakaozaliwa.
Wasimame na kuwaambia wana wao
Wamwekee Mungu tumaini lao.
Wala wasiyasahau matendo ya Mungu,
Bali wazishike amri zake.(K)
3. Naam, wasiwe kama baba zao,
Kizazi cha ukaidi na uasi.
Kizazi kisichojitengeneza moyo,
Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu. (K)
SHANGILIO: Yn.17:17
Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya.
INJILI: Mk.2:1-12
Baada ya siku Yesu akaingia tena Kapernaumu. Ikasikiwa ya kwamba Yesu alikuwa nyumbani. Wakakusanyika
watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake. Wakaja watu wakimletea mtu
mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne. Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano,
waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye
kupooza. Naye Yesu, alipoiona Imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa
dhambi zako. Na baadhi ya waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao, Mbona
huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu? Mara
Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi
mioyoni mwenu? Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka,
ujitwike godoro lako, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya
kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza), Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende
nyumbani kwako. Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu
wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, Mwanao alihukumiwa kifo cha msalaba
kwa sababu ya ugumu wa mioyo ya baadhi ya wale
aliowahubiria neno lako. Sasa tunakuomba:-
Kiitikio: Mungu wa huruma, utusikie.
l. Viongozi wote wa Kanisa waongezewe bidii ya
kuwahubiria watu Habari Njema ya toba, iletayo
ondoleo la dhambi. Ee Bwana.
2. Uwatie moyo watawala wote wa dunia wanaojitahidi
kuwaongoza raia wao katika haki na ukweli. Ee Bwana.
3. Umjalie kila mmoja wetu kuitii sauti yako
inayotujia kupitia viongozi wetu wa dini na serikali
au mtu yeyote mwenye nia njema. Ee Bwana.
4. Sisi sote tujaliwe moyo na ari ya kuwasaidia wenzetu
wenye shida, wapate kukutana na Mwanao na
kuondolewa kero zao. Ee Bwana.
5. Uwapokee na kuwaingiza rahani mwako ndugu zetu
marehemu. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo, aliye Bwana
na Mwokozi wetu. Anayeishi na kutawala milele na
milele. Amina.