IJUMAA JUMA 22 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: 1Kor.4:1-5
Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu. Lakini, kwangu mimi, si kitu kabisa nihukumiwe na ninyi, wala kwa hukumu ya kibinadamu, wala sijihukumu hata nafsi yangu. Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo; ila anihukumuye mimi ni Bwana. Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.37:3-6,27,28,39-40(K)39
1. Umkabizi Bwana njia yako,
Pia umtumaini, naye atafanya.
Atajitokeza haki yako kama nuru,
Na hukumu yako kama adhuhuri.

(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.

2. Umtumaini Bwana ukatende mema,
Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
Naye atakupa haja za moyo wako. (K)

3. Jiepue na uovu, utende mema,
Na kukaa hata milele.
Kwa kuwa Bwana hupenda haki,
Wala hawaachi watauwa wake. (K)

4. Na wokovu wa wenye haki una Bwana;
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa;
Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa;
Kwa kuwa wamemtumaini Yeye. (K)

SHANGILIO: Zab.25:4,5
Aleluya, aleluya!
Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako.
Aleluya!

INJILI: Lk.5:33-39
Mafarisayo na waandishi walimwambia Yesu, Wanafunzi wa Yohane hufunga mara nyingi, na kuomba dua; na kadhalika wanafunzi wa Mafarisayo; lakini wanafunzi wako hula na kunywa! Lakini Yesu akawaambia, Je! Mwaweza kuwafanya wafunge walioalikwa arusini, akiwapo bwana arusi pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku zile. Akawaambia na mithali, Hakuna akataye kiraka cha vazi jipya na kukitia katika vazi kuukuu; na kama akitia, amelikata lile jipya, na kile kiraka cha vazi jipya hakilingani na lile vazi kuukuu. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama akitia, ile divai mpya itavipasua vile viriba, divai yenyewe itamwagika, na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya sharti kutiwa katika viriba vipya. Wala hakuna anywaye divai ya kale akatamani divai mpya; kwa kuwa asema, Ile ya kale ndiyo iliyo njema.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, tumwombe Mungu ambaye pamoja na Mwanae, Yesu Kristo, anautawala kabisa ulimwengu huu mpya:-

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umjalie Baba Mtakatifu wetu F., kumwakilisha kiaminifu Kristo Mwanao, aliye kichwa cha Kanisa, ili watu wako watubu na kupata wokovu. Ee Bwana.

2. Upende kuwakumbusha daima watawala wa dunia kuwa vitu vyote viliumbwa kwa njia ya Kristo na kwa ajili yake. Ee Bwana.

3. Kwa njia ya amani ambayo Mwanao Yesu Kristo alifanya kwa damu yake msalabani, utujalie utimilifu wote na kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake. Ee Bwana.

4. Utujalie kujiandaa vema kwa siku ya hukumu, ambapo ya giza yatamulikwa, mashauri ya moyo yatadhihirishwa na kila mtu atapata sifa yake kwako. Ee Bwana.

5. Kwa mastahili ya mateso, kifo na ufufuko wa Mwanao Yesu Kristo, marehemu wetu wapewe uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu, unayetaka tufunge wakati wa kufaa kwa wokovu wetu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.