IJUMAA JUMA 23 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: 1Kor.9:16-19,22-27
Ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu
nisipoihubiri Injili! Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si
kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili. Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo,
nitaitoa Injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.
Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi
zaidi. Kwa unyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote,
ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu. Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili
kuishiriki pamoja na wengine. Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga
mbio wote lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. Na kila ashindanaye
katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo;
bali sisi tupokee taji isiyoharibika. Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napiga
ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe,
nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.84:2-5,7,11
1. Nafsi yangu imeziona shauku nyua za Bwana,
Naam, na kuzikondea.
Moyo wangu na mwili wangu
Ninamlilia Mungu aliye hai.
(K) Maskani zao zapendeza kama nini, Ee Bwana wa majeshi.
2. Shomoro naye ameona nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia kioto,
Alipoweka makinda yake,
Kwenye madhabahu zako, Ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu. (K)
3. Heri wakaao nyumbani mwako,
Wanakuhimidi daima.
Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.
Huendelea toka nguvu hata nguvu,
Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu. (K)
4. Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao,
Bwana atatoa neema na utukufu.
Hatawanyima kitu chema
Hao waendao kwa ukamilifu. (K)
SHANGILIO: Mt.11:25
Aleluya, aleluya!
Nakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha
wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya!
INJILI: Lk.6:39-42
Yesu aliwaambia wanafunzi wake mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia
shimoni wote wawili? Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu
hulingana na mwalimu wake. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako,
na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenye huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako,
Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo
ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafikiri wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe,
ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, wema haupaswi kuuzidi uwezo. Ndiyo maana
kipofu hawezi kumwongoza kipofu mwenzake. Tumwombe
Mungu neema zake.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwatie nguvu Papa wetu F.,
Askofu wetu F. na
Mapadre wote uliowaweka katika utumishi wako
mtakatifu. Ee Bwana.
2. Pamoja na Raisi wetu kuwa huru kwa watu wote,
umjalie roho ya ujasiri, apate kuwa hali zote kwa
watu wote; ili afanye mambo yote kwa ajili ya
manufaa ya wote. Ee Bwana.
3. Uwaongoe wazushi, wapinga dini na wote wenye
mwenendo mbaya wa maisha, wapate kuishi kadiri
ya kweli yako. Ee Bwana.
4. Uamshe ndani ya wanafunzi wote ari ya kutoridhika
na vyeti tu, bali wajiandae kuhitimu vizuri kitaaluma
na kimaadili, ili wasiwe viongozi vipofu. Ee Bwana.
5. Uwapokee ndugu zetu marehemu na kuwapa rehema
na amani ya kudumu huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tuache unafiki, uyapokee maombi
yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.