IJUMAA JUMA 24 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: 1Kor. 15:12–20
Ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu? Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka; tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwenu ni bure na Imani yetu ni bure. Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, Imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.17:1,6-8,15(K)15
1. Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiyotoka katika midomo ya hila.

(K) Nishibishwe, Ee Bwana, kwa sura yako.

2. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika,
Utege sikio lako ulisikie neno langu.
Dhihirisha fadhili zako za ajabu,
Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia;
Kwa mkono wako wa kuume
Uwaokoe nao wanaowaondokea. (K)

3. Unilinde kama mboni ya jicho,
Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;
Bali mimi nikutazame uso wako katika haki,
Niamkapo nishibishwe kwa sura yako. (K)

SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya!

INJILI: Lk.8:1-3
Yesu alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yohana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu, twakiri kuwa utaua pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa vile tunasongwa na vishawishi na magumu mengi katika maisha haya, tunathubutu kukuomba tukisema.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwawezeshe viongozi wetu wa Kanisa kuvipiga vita vile vizuri vya imani, na hivi kuwatia moyo waamini wao katika kuilinda imani na kuyashinda majaribu. Ee Bwana.

2. Wote wanaotoa huduma kwa jamii wajaliwe kufuata haki, upendo, saburi na upole. Ee Bwana.

3. Utuepushe sisi sote na tamaa ya fedha ambayo ni shina la uharibifu na hatarishi kwa imani. Ee Bwana.

4. Kwa ajili ya wenye mashaka juu ufufuo wa wafu, ili waongoke kutoka dhambini na kumwendea Kristo aliye limbuko lao waliolala. Ee Bwana.

5. Uwajalie ndugu zetu marehemu uzima wa milele walioitiwa wakiwa tangu hapa duniani. Ee Bwana.

Ee Mungu uliyetaka msalaba uwe alama ya ushindi wa Mwanao, Yesu Kristo, dhidi ya dhambi, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya huyo Kristo Bwana wetu. Amina.