IJUMAA JUMA 25 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Mhu.3:1-11
Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa,
na wakati wa kufa; wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa; wakati wa kuua, na
wakati wa kupoza; wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; wakati wa kulia, na wakati wa kucheka;
wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe;
wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza;
wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa; wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; wakati wa
kunyamaza, na wakati wa kunena; wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; wakati wa vita, na
wakati wa amani. Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo? Nimeiona
taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake. Kila kitu amekifanya kizuri kwa
wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza
kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.144:1-4(K)1
1. Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu,
Mhisani wangu na boma langu,
Ngome yangu na mwokozi wangu,
Ngao yangu niliyemkimbilia.
(K) Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu.
2. Ee Bwana, mtu ni kitu gani hata umjue?
Na binadamu hata umwangalie?
Binadamu amefanana na ubatili,
Siku zake ni kama kivuli kipitacho. (K)
SHANGILIO: Zab.119:135
Aleluya, aleluya!
Umwangazie mtumishi wako uso wako, na kunifundisha amri zako.
Aleluya!
INJILI: Lk.9:18-22
Yesu alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwapo pamoja naye, akawauliza, Je!
Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani? Wakamjibu wakisema, Yohane Mbatizaji; lakini wengine,
Eliya; na wengine kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. Akawaambia, Nanyi mwasema ya
kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu. Akawaonya, akawakataza
wasimwambie mtu neno hilo. Akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa
na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, tumwombe Mungu anayeruhusu hata mateso
kutokea katika maisha na katika utume wetu. Ee Bwana
Mungu, twakuomba.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie viongozi wote wa Kanisa uhodari katika
kufundisha imani ya kweli, kuilinda na kuitetea,
hasa katika ulimwengu huu wa sasa. Ee Bwana.
2. Wewe uliyekifanya kila kitu kizuri kwa wakati
wake, uwajalie viongozi wetu wa serikali
kuzitekeleza ahadi zao kiaminifu na kwa wakati wake. Ee Bwana.
3. Wasiokujua Wewe Mungu katika nafsi ya Mwanao
Yesu Kristo wajaliwe wongofu, ili Wewe peke yako
utukuzwe mahali pote. Ee Bwana.
4. Utujalie baraka na ulinzi wako sote tunaoingia
mahali pako patakatifu na kulitukuza jina lako. Ee Bwana.
5. Uwapokee kwako marehemu walioukiri umungu na
ukuu wako wakiwa hapa duniani. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyemtukuza Mwanao Yesu Kristo hata katika
mateso, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya huyo Kristo
Bwana wetu. Amina.