IJUMAA JUMA 26 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Ayu.38:1,12-21,40:3-5
Ndipo Bwana alimjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Je! Umeiamuru asubuhi tangu
siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake? Yapate kuishika miisho ya nchi, waovu
wakung’utwe wakawe mbali nayo? Hubadilika mfano wa udongo chini ya muhuri, vitu vyote vinatokea
kama mavazi. Na waovu nuru yao huzuiliwa isiwafikie, na mkono ulioinuka huvunjika. Je! Umeziingia
chemchemi za bahari, au umetembea mahali pa siri pa vilindi? Umeyafahamu mapana ya dunia? Haya! Sema,
ikiwa unayajua hayo yote. Iko wapi njia ya kuyafikia makao ya nuru? Na giza pia, mahali pake ni wapi?
Upate kuipeleka hata mpaka wake, upate kuelewa na mapito ya kuiendea nyumba yake? Hukosi unajua, maana
ulizaliwa wakati huo, na hesabu ya siku zako ni kubwa! Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si
kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu. Nimenena mara moja, nami sitajibu;
naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.139:1-3,7-10,13-14(K)13
1. Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu:
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.
(K) Uniongoze Bwana, katika njia ya milele.
2. Niende wapi nijiepushe na roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko;
Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. (K)
3. Ningezitwaa mbawa za asubuhi,
Na kukaa pande za mwisho za bahari;
Huko nako mkono wako utaniongoza,
Na mkono wako wa kuume utanishika. (K)
4. Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. (K)
SHANGILIO: Yn.14:5
Aleluya, aleluya!
Bwana anasema: mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, mtu haji kwa Baba,
ila kwa njia ya mimi.
Aleluya!
INJILI: Lk.10:13-16
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza
hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi
katika nguo za kigunia na majivu. Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili
adhabu zake kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu.
Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi
amkataa yeye aliyenituma.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Mungu ametupatia Wachungaji katika Kanisa
wapate kutuongoza badala yake. Tuombe neema yake
Mungu tukisema.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Maaskofu, Mapadre na Makatekista wetu wazidi
kutangaza msamaha wako, ili wakosefu waache njia
zao mbaya na kukurudia Wewe, Mungu msamehevu. Ee Bwana.
2. Uwe pamoja na viongozi wa serikali, hasa wale
wanaohitaji msaada wako, katika kukabiliana na
changamoto za kiutawala, kwa manufaa ya raia
wao na taifa zima. Ee Bwana.
3. Waamini wawe wasikivu kwa viongozi wao wa dini
ili, kwa njia yao, wapate kukutana nawe, kukujua
zaidi na kukutumikia kwa uchaji. Ee Bwana.
4. Umjalie kila mmoja wetu moyo wa toba, tupate kutubu
dhambi zetu, kukusudia kuziacha na kuwasamehe
wenzetu. Ee Bwana.
5. Kwa huruma yako, ndugu zetu marehemu wapewe
uzima mpya huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uyapokee maombi haya na yale ambayo
hatukuyataja. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.