IJUMAA JUMA 27 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Gal.3:7-14
Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Na andiko, kwa vile lilivyoona
tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani,
kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu
aliyekuwa mwenye imani. Kwa maana wale walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa,
Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye. Ni Dhahiri
ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa
imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. Kristo alitukomboa katika
laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu
aangikwaye juu ya mti; ili kwamba Baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristu, tupate
kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.111:1-6(K)5
Aleluya.
1. Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
Matendo ya Bwana ni makuu,
Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo.
(K) Alikumbuka agano lake milele.
2. Kazi yake ni heshima na adhama,
Na haki yakaa milele.
Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu,
Bwana ni mwenye fadhili na rehema. (K)
3. Amewapa wamchao chakula,
Atalikumbuka agano lake milele.
Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake,
Kwa kuwapa urithi wa mataifa. (K)
SHANGILIO: 1Sam.3:9,Yn.6:68
Aleluya, aleluya!
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia; wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya!
INJILI: Lk.11:15-26
Wengine wa makutano walisema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu,
wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia. Kila ufalme uliofitinika
wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa shetani naye
amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa
pepo kwa Beelzebuli. Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani?
Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu,
basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo
nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda,
amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake. Mtu ambaye si pamoja
nami yu kinyume changu; na mtu aliyekusanya pamoja nami hutawanya. Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia
mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitarudia nyumba yangu niliyotoka.
Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu
kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya
kwanza.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Yesu umesema: “Mtu ambaye si pamoja nami yu
kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami
hutawanya.” Basi tunakuomba.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F., Maaskofu na viongozi
wote wa Kanisa wabaki imara, katika kuifundisha
na kuitetea imani sahihi, dhidi ya waasi na
wanaolikufuru jina lako. Ee Bwana.
2. Wote wenye mamlaka katika jamii wawe chachu
nzuri, wapate kuigwa na watu wao katika kujiandaa
kwa siku ya ujio wako. Ee Bwana.
3. Utuepushe na pepo wabaya na, kwa nguvu ya
Roho wako Mtakatifu, utuimarishe katika
kupambana na maadui wa imani yetu kwako. Ee Bwana.
4. Tunawaombea wenye imani haba, ili waepukane na
dhambi ya kumkufuru Roho wako Mtakatifu; wala
wasiwakwaze wanyofu wa moyo. Ee Bwana.
5. Wote waliofariki dunia watakaswe dhambi zao na
kufikishwa huko kwako binguni. Ee Bwana.
Ee Yesu uliyetupenda mpaka kufa, uyapokee maombi
yetu. Unayeishi na kutawala daima na milele. Amina.