IJUMAA JUMA 29 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Efe.4:1-6
Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa;
kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi
umoja wa Roho katia kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini
moja la wito wenu. Bwana mmoja, Imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye
juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.24:1-6(K)6
1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.
2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili,
Wala hakuapa kwa hila.(K)
3. Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)
SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya!
INJILI: Lk.12:54-59
Yesu aliwaambia makutano pia, kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua
inakuja; ikawa hivyo. Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo. Enyi
wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya?
Na mbona ninyi wenyewe kwa nafsi zenu hamwamui yaliyo haki? Maana, unapofuatana na mshitaki wako
kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidi kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi;
yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani.
Nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa kwake yeye atakaye kutenda lililo jema
lipo baya lisilotakiwa, tuombe neema ya Mungu.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Ili Askofu wetu F. na wahubiri wote wa neno lako
wasichoke kukemea maovu na kuhamasisha matendo
mema yaletayo uzima wa milele. Ee Bwana.
2. Ili hata watawala wa dunia watambue kuwa amani ya
kweli hutokana na kufurahia sheria ya Mungu kwa
utu wa ndani. Ee Bwana.
3. Ili, kwa kuepukana na unafiki, tuokolewe na mauti
yaletwayo na mambo ya kimwili. Ee Bwana.
4. Ndugu, marafiki na wana ndoa waliofarakana,
wajirudi na kuenenda inavyostahili wito wao kwa
unyenyekevu; wakichukuliana katika upendo; na
kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika
kifungo cha amani. Ee Bwana.
5. Ili ndugu zetu waliofariki dunia wafike kwako
mbinguni na kufurahi nawe milele. Ee Bwana.
Ee Mungu Baba uliyekubali Mwanao afe msalabani japo
hakuwa na kosa lolote, uyapokee maombi yetu. Kwa njia
ya huyo Kristo Bwana wetu. Amina.