IJUMAA JUMA 2 MAJILIO
MASOMO

SOMO 1: Isa.48:17-19
Bwana, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi: Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata. Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo Amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari; tena wazao wako wangalikuwa kama mchanga, na hao waliotoka katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingaliondolewa, wala kufutwa mbele zangu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.1:1-4,6
1. Heri mtu yule asiyekwenda,
Katika shauri la wasio haki,
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. (K)

(K) Akufuataye, Bwana, atakuwa na nuru ya uzima.

2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa,
Kandokando ya vijito vya maji.
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)

3. Sivyo walivyo wasio haki,
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)

Shangilio
Aleluya, aleluya,
Bwana atakuja, nendeni kumlaki, Yeye ni mfalme wa Amani.
Aleluya.

INJILI: Mt.11:16-19
Siku ile, Yesu aliwaambia makutano: Lakini nitakifananisha na nini kizazi hiki? Kimefanana na watoto wanaokaa sokoni, wanaowaita wenzao, wakisema, Tuliwapigia filimbi, wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia. Maana Yohane alikuja, hali wala hanywi, wakasema, Yuna pepo. Mwana wa Adamu alikuja, akila na kunywa, wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa amani yetu hupatikana katika kuyatimiza mapenzi ya Mungu, tumwombe tukisema:

Kiitikio: Mungu wa huruma, utusikie.
1. Utukumbushe daima kuwa mafundisho yako huleta faida kimwili na kiroho na utupe moyo wa kuyashika mafundisho hayo kwa dhati. Ee Bwana.

2. Utuoneshe njia iongozayo kwenye ukweli wako. Ee Bwana.

3. Ahadi yako ya kuwa na wazao wengi kama mchanga imesongwa na magonjwa na kila hatari. Utuhurumie na utukinge na majanga hayo. Ee Bwana.

4. Utujalie hekima imara kusudi tusiyumbishwe na malimwengu, ili Mkombozi wetu ajapo atukute tukikesha. Ee Bwana.

Ee Baba wa mbinguni, Mwanao ni rafiki wa watoza ushuru na wenye dhambi. Utujalie nasi kuwapenda wakosefu na kuwaandaa kwa ujio wake. Kwa huyo Kristo Bwana wetu. Amina.