IJUMAA JUMA 2 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.8:6–13
Kuhani wetu sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora,
lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora. Maana kama lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi
isingalitafutwa kwa lile la pili. Maana, awalaumupo, asema, Angalia, siku zinakuja, asema Bwana,
nami nitawatimizia nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda agano jipya; halitakuwa kama agano lile
nililoagana na baba zao, katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri.
Kwa sababu hawakudumu katika agano langu, Mimi nami sikuwajali, asema Bwana. Maana hili ndilo agano
nitakaloagana na nyumba ya Israeli baada ya siku zile asema Bwana; nitawapa sheria zangu katika nia
zao, na katika mioyo yao nitaziandika; nami nitakuwa Mungu kwao, nao watakuwa watu wangu. Nao
hawatafundishana kila mtu na jirani yake, na kila mtu na ndugu yake, akisema, Mjue Bwana; kwa maana
wote watanijua, tangu mdogo wao hata mkubwa wao. Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, na dhambi zao
sitazikumbuka tena. Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini
kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.85:7,9–13 (K)10
1. Ee Bwana, utuoneshe rehema zako,
Utupe wokovu wako.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.
(K) Fadhili na kweli zimekutana.
2. Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na Amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)
3. Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)
SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo,
awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.
INJILI: Mk.3:13-19
Yesu alipanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili,
wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo. Akawaweka
wale Thenashara; na Simoni akampa jina la Petro; na Yakobo, mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye
Yakobo, akawapa jina la Boanerge, maana yake, wana wa ngurumo; na Andrea, na Filipo, na
Bartholomayo, na Mathayo, na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Thadayo, na Simoni Mkananayo,
na Yuda Iskariote, ndiye aliyemsaliti.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu zangu, Mungu ameweka nasi Agano Jipya na la
milele kwa sadaka ya Yesu Kristo msalabani. Basi, katika
adhimisho hili tumwombe tukisema;-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Viongozi wa Kanisa wadumishe mfano bora katika
kuyashika maagano matakatifu kadiri ya mwito wako
uletao wokovu. Ee Bwana.
2. Wote wenye mamlaka juu ya watu wako waoneshe
kukujali wewe Mungu kwa kuwatumikia vema watu
wanaowaongoza. Ee Bwana.
3. Kila mmoja wetu abebe msalaba wake kwa kushika
sheria zenye lengo la kutukomboa na kutuletea uzima
mpya. Ee Bwana.
4. Utujalie msamaha hata kwa maadui zetu, ili nao
wapate kukuongokea wewe na kupata wokovu. Ee
Bwana.
5. Kwa mastahili ya mateso, kifo na ufufuko wa Mwanao
Yesu Kristo, ndugu zetu marehemu wasamehewe
dhambi zao, wapate kuishi nawe milele. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.