IJUMAA JUMA 31 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Flp.3:17-4:1
Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi. Maana
wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi,
kuwa ni adui za msalaba wa Kristo; mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u
katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani. Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka
huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate
kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote
viwe chini yake. Basi, ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji
yangu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.122:1-5(K)1
1. Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.
(K) Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana
2. Ee Yerusalemu uliyejengwa Kama mji ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila, Kabila za Bwana; (K)
3. Ushuhuda kwa Israeli, Walishukuru jina la Bwana.
Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
Viti vya enzi vya mbari ya Daudi.(K)
SHANGILIO: Yn.14:23
Aleluya, aleluya!
Mtu akinipenda, atalishika neno langu,
na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake.
Aleluya!
INJILI: Lk.16:1-8
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu
alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake. Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia
juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena. Yule wakili akasema moyoni
mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya. Najua
nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao. Akawaita wadeni wa
bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu? Akasema, Vipimo mia vya mafuta.
Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini. Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani?
Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini. Yule bwana akamsifu wakili
dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa
na busara kuliko wana wa nuru.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, kwa unyenyekevu na unyofu wa moyo,
tumwombe Mungu katika shida zetu.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Baba Mtakatifu wetu F., Maaskofu na Mapadre wetu
wote waifanyie Injili yako kazi ya ukuhani, kusudi
Mataifa wawe sadaka yenye kibali mbele yako. Ee
Bwana.
2. Wote waliodhaminiwa kazi ya utunzaji mali kwa niaba
ya wengine katika jamii, wajaliwe kuifanya kazi hiyo
kwa busara yenye kuhesabiwa haki. Ee Bwana.
3. Utujalie unyenyekevu, tupate kutambua uwepo wako
wa daima katika shughuli zetu za kila siku, na tuone
fahari kuitukuza kazi yako. Ee Bwana.
4. Uimarishe utashi wetu dhidi ya maadui wa Msalaba
wa Mwanao, Yesu Kristo; ili fahari yetu iwe katika
kuacha anasa za dunia zinazopingana na wenyeji
wetu huko mbinguni. Ee Bwana.
5. Uwakaribishe ndugu zetu marehemu katika ufalme
wako wa mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka unyofu wa moyo katika mahusiano
yetu, uyapokee maombi haya. Kwa njia ya Kristo Bwana
wetu. Amina.