IJUMAA JUMA 32 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: 2Yoh.1:4-9
Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile
tulivyopokea amri kwa Baba. Na sasa, mama, nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali
ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane. Na huu ndio upendo; tuenende kwa kuzifuata
amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo. Kwa
maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili.
Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda,
bali mpokee thawabu timilifu. Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye
hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:1-2,10-11,17-18(K)1
1. Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote.
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.
2. Kwa moyo wangu wote nimekutafuta,
Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,
Nisije nikakutenda dhambi. (K)
3. Umtendee mtumishi wako ukarimu,
Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
Unifumbue macho yangu niyatazame
Maajabu yatokayo katika sheria yako. (K)
SHANGILIO: Zab.119:28,33
Aleluya, aleluya!
Unitie nguvu sawasawa na neno lako, Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako.
Aleluya!
INJILI: Lk.17:26-37
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika
siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku
ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama
ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda
na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulikunya moto na kibiriti kutoka mbinguni
vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. Katika
siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na
kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu yeyote atakaye kuiponya
nafsi yake, ataiangamiza; na yeyote atakayeiangamiza ataiponya. Nawaambia, usiku huo watu wawili
watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga
pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia. Ulipo
mzoga, ndipo watakapokutanika tai.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, Mwanao amesema ulipo mzoga ndipo
watakapokutanika tai. Sisi tuliokusanyika hapa kwa
jina lake, twakuomba:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Viongozi wetu wa Kanisa wasichoke kuwakumbusha
watu wako juu ya ujio wa Mwanao siku ya mwisho. Ee Bwana.
2. Utawale mioyo ya viongozi wote wa serikali, ili
wasiruhusu nchini dini haramu au vikundi vya
matapeli na wadanganyifu; bali wasimamie utu
wema, haki, ukweli na amani. Ee Bwana.
3. Wote wasiokufahamu wapate kukiri uwepo wako,
walao kwa kuvitazama viumbe vizuri vinavyoonekana,
na kwa kuzichungulia taratibu za viumbe hivyo. Ee Bwana.
4. Sisi tunaomwamini Mwanao Yesu Kristo tujaliwe
kuikiri imani yetu kwa maneno na matendo yetu
mema siku zote. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wasamehewe dhambi zao na
kufikishwa kwako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tuwe tayari hata kuziangamiza nafsi
zetu kwa ajili yako, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.