IJUMAA JUMA 33 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Ufu.10:8-11
Mimi, Yohane, nilisikia sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema,
Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu
ya bahari na juu ya nchi. Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo.
Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako
kitakuwa kitamu kama asali. Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila;
nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa
uchungu. Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:14,24,72,103,111,131(K)103
1. Nimeifurahia njia ya shuhuda zako,
Kana kwamba ni mali mengi.
Shuhuda zako ndizo furaha yangu,
Na washauri wangu.
(K) Mausia yako ni matamu sana kwangu.
2. Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
Mausia yako ni matamu sana kwangu,
Kupita asali kinywani mwangu. (K)
3. Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele,
Maana ndizo changamko la moyo wangu.
Nalifunua kinywa changu nikatweta,
Maana naliyatamani maagizo yako. (K)
SHANGILIO: 2Kor.5:19
Aleluya, aleluya!
Mungu alikuwa ndani ya Kristu, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake,
ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya!
INJILI: Lk.19:45-48
Yesu aliingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, Imeandikwa,
Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi. Naye akawa
akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa
wakitafuta njia ya kumwangamiza; wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye,
wakimsikiliza.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tupeleke sasa maombi yetu kwa Mungu anayependa tuitumie vema nyumba yake ya
sala kwa manufaa yetu sisi wenyewe.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Maaskofu na Mapadre wetu wasichoke kutolea dhabihu ya wokovu na shukrani
altareni pako. Ee Bwana.
2. Watawala wote duniani wajenge mazingira rafiki kwa uenezaji Injili na utoaji
unabii juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi. Ee Bwana.
3. Wote wakuaminio wakuabudu kifudifudi, wakipaza sifa mbinguni, kwako Wewe unayewafanikisha
katika maisha. Ee Bwana.
4. Utujalie sisi sote kushika kiaminifu na kitakatifu Siku yako Bwana, na Sikukuu zote
ulizotuamuru kwa ajili ya wokovu wetu. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wapate kitulizo na faraja, kwa
kusamehewa dhambi na kupewa uzima wa milele. Ee Bwana.
Ee Mungu, uyapokee maombi haya tuliyokutolea. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.