IJUMAA JUMA 34 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO Ufu.20:1-4,11-21:2
Mimi, Yohane, niliona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa
mkononi mwake. Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga
miaka elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akamtia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa
tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache. Kisha nikaona viti
vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili
ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake,
wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai,
wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu. Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye
juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu,
wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine
kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika
vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu
zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Mauti na Kuzimu
zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu
yeyote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto. Kisha nikaona
mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari
tena. Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa
tayari, kama bibi arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.84:2-5,7(K)Ufu.21:3
1. Nafsi yangu imeziona shauku nyua za Bwana,
Naam, na kuzikondea.
Moyo wangu na mwili wangu
Vinamlilia Mungu aliye hai. (K)
(K) Mungu anakuwa pamoja na watu.
2. Shomoro naye ameona nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia kioto,
Alipoweka makinda yake, kwenye madhabau zako,
Ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu. (K)
3. Heri wakaao nyumbani mwako,
Wanakuhimidi daima.
Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake. (K)
SHANGILIO: Zab.19:8.
Aleluya, aleluya!
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya!
INJILI: Lk.21:29-33
Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano, Utazameni mtini na miti mingine yote. Wakati iishapo
kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu. Nanyi
kadhalika, mwonapo yamekwisha kuwa karibu. Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea,
tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu. Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo
yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, mamlaka, na utukufu, na ufalme ni vya Mungu wetu, naye anastahili
kutumikiwa na watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Kwa hiyo, tumwombe.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa
lako wajaliwe kuwa mawakili waaminifu zaidi wa Mwanao, ili watu wapate kumtegemea
zaidi katika maisha yao. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia watambue kuwa Wewe ndiwe mwenye mamlaka yote na ya milele, na
ufalme wako hautaangamizwa milele. Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote kuzisoma vema na kwa jicho la imani ishara za nyakati, na
kujiandaa vema kwa ujio wa hukumu ya mwisho. Ee Bwana.
4. Uyafute makosa yetu katika vitabu vyako vya hukumu ili, utakapowahukumu
watu kadiri ya matendo yao, tupate kuhesabiwa haki kwa huruma yako. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wasamehewe dhambi zao, wapate kuurithi uzima wa
milele mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetimiza ukombozi wetu kwa mateso, kifo na ufufuko wa Mwanao,
uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.