IJUMAA JUMA 3 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.10:32-39
Zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu;
pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendewa hayo. Maana
mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang'anywa mali zenu,
mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo. Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana
una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi.
Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia. Lakini mwenye haki wangu ataishi
kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na
kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.37:3-6,23-24,39-40 (K)39
1. Umtumaini Bwana ukatende mema,
Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
Naye atakupa haja za moyo wako.
(K) Wokovu wa mwenye haki una Bwana.
2. Umkabidhi Bwana njia yako,
Pia umtumaini, naye atafanya.
Ataitokeza haki yako kama nuru,
Na hukumu yako kama adhuhuri. (K)
3. Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana,
Naye aipenda njia yake.
Ajapojikwaa hataanguka chini,
Bwana humshika mkono na kumtegemeza. (K)
4. Na wokovu wa wenye haki una Bwana;
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa;
Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa;
Kwa kuwa wamemtumaini Yeye. (K)
SHANGILIO: 1The.2:13
Aleluya, aleluya,
Lipokeeni neo la Mungu si kama vile ujumbe wa binadamu,
bali kama ujumbe wa Mungu,
Aleluya.
INJILI: Mk.4:26-34
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi;
akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi
huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara
atapeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie
katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko
mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga,
ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. Kwa mifano mingi ya
namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; wala pasipo mfano hakusema
nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa sisi tu miongoni mwa walioipokea
imani iletayo wokovu, tumwombe Mungu tukisema:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Kwa nguvu na fumbo la Msalaba wa Mwanao, Yesu
Kristo, viongozi wetu wa Kanisa watoe mfano mzuri
katika kuikiri imani yetu, kustahimili mashutumu na
dhiki. Ee Bwana.
2. Wote wenye madaraka wapiganie haki za watoto
kwani, pamoja na udogo wao, ni binadamu kamili
na warithi halali wa dunia na mbingu. Ee Bwana.
3. Utuepushe sisi sote na tamaa za mwili na matumizi
mabaya ya madaraka, tupate kudumisha haki na
usawa, hasa kwa wanyonge. Ee Bwana.
4. Utuongezee ari ya kulisikia neno lako na kuwahubiria
wengine kwa saburi, ili tupate wokovu tulioahidiwa.
Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wapokelewe mbele ya kiti chako cha
enzi huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, mwenye haki wako ataishi kwa imani. Uyapokee
hayo tukuombayo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.