IJUMAA JUMA 4 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.13:1-8
Upendano wa ndugu na udumu. Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha
malaika pasipo kujua. Wakumbukeni hao waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao; na hao wanaodhulumiwa,
kwa vile ninyi nanyi mlivyo katika mwili. Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa
maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na
vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata
twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Wakumbukeni wale
waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo
wao, iigeni imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.27:1,3,5,8-9 (K)1
1. Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu
2. Jeshi lijapojipanga kupigana nami,
Moyo wangu hautaogopa.
Vita vijaponitokea,
Hata hapo nitatumaini. (K)
3. Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya,
Atanisitiri katika sitara ya hema yake,
Na kuniinua juu ya mwamba. (K)
4. Bwana, uso wako nitautafuta.
Usinifiche uso wako,
Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira.
Umekuwa msaada wangu, usinitupe,
Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. (K)
SHANGILIO: Zab.130:5
Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana,
na neno lake nimelitumainia.
Aleluya.
INJILI: Mk.6:14-29
Mfalme Herode akasikia habari; kwa maana jina lake lilikuwa kutangaa, akasema, Yohana Mbatizaji
amefufuka katika wafu, na kwa hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake. Wengine walisema, Ni Eliya.
Wengine walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii. Lakini Herode aliposikia, alisema,
Yohana, niliyemkata kichwa, amefufuka. Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata
Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; kwa
sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa
akimvizia, akataka kumwua, asipate. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki,
mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa
furaha. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu
wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia,
akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana,
Niombe lo lote utakalo, nitakupa. Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu.
Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mara akaingia
kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana
Mbatizaji. Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi
karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda,
akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana
akampa mamaye. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tumwombe Mungu aliyemtuma Mwanae Yesu
Kristo awe kielelezo cha Upendo tukisema.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa
lako wadumu katika kuwakumbusha waamini wajibu
wa kuuishi upendo wako. Ee Bwana.
2. Wote wenye dhamana ya uongozi katika jamii zetu
wajaliwe upendo na waepushwe na tamaa ya fedha
katika utoaji wa huduma zao za kijamii. Ee Bwana.
3. Tunawaombea wenye karama mbalimbali, ili daima
watoe mchango wao kwa Kanisa, lipate kukuhimidi
kila siku, kukuimbia kwa sauti tamu na kukupatia
utukufu unaostahili. Ee Bwana.
4. Kila mmoja wetu avutwe na moyo wa upendo na
huduma kwa wageni, yatima, wajane na wenye shida
kwani, katika hao, twakutana nawe. Ee Bwana.
5. Kwa mastahili ya upendo wa Mwanao, Yesu Kristo,
uliofikia kipeo chake msalabani, marehemu wetu
wapate uzima wa milele mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyempatia Mt. Yohane Mbatizaji neema ya
unabii usio na woga wala upendeleo, uyapokee maombi
yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.