JUMATATU JUMA 6 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.11:1–9
Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja. Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona
nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali tukayachome
moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. Wakasema, Haya, na tujijengee
mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa
nchi yote. Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. Bwana akasema, Tazama,
watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na hayo ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa
hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili
wasisikilizane maneno wao kwa wao. Basi Bwana akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote;
wakaacha kuujenga ule mji. Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo Bwana
alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko Bwana akawatawanya waende usoni pa nchi yote.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.33:10–15 (K)12
1. Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa,
Huyatangua makusudi ya watu.
Shauri la Bwana lasimama milele,
Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.
(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.
2. Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
Toka mbinguni Bwana huchungulia,
Huwatazama wanadamu wote pia. (K)
3. Toka mahali pake aketipo,
Huwaangalia wote wakaao duniani.
Yeye aiumbaye mioyo yao wote
Huzifikiri kazi zao zote. (K)
SHANGILIO: Zab.119:13
Aleluya, aleluya!
Umwangazie mtumishi wako uso wako,
na kunifundisha amri zako.
Aleluya!
INJILI: Mk.8:34–9:1
Yesu aliwaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane
mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza,
na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha. Kwa
kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala
ya nafsi yake? Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi
na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na
malaika watakatifu. Akawaambia, Amin, nawaambia, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja
mauti kabisa, hata watakapouona ufalme wa Mungu umekuja kwa nguvu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kumfuata Yesu Kristo maana yake kuwa tayari
kuupokea na kuubeba msalaba na hata kuwa tayari kufa
kwa ajili yake. Wajibu huu ni wa muhimu sana. Tuombe:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Viongozi wa Kanisa wadumishe lugha moja ya upendo,
ili Injili yako ienee duniani kote kwa nguvu
ya Roho wako Mtakatifu. Ee Bwana.
2. Wote wenye mamlaka wajaliwe busara na utawala
bora, ili mali za ulimwengu huu ziwe kwa faida ya
watu wako kimwili na kiroho. Ee Bwana.
3. Utuepushe sisi sote na kiburi chenye mwelekeo wa
kukukosoa Wewe na kazi yako ya uumbaji. Ee Bwana.
4. Umjalie kila mmoja wetu kuiishi imani yake kwa
matendo, tupate kuhesabiwa haki kama
ulivyomfanyia baba yetu Ibrahimu. Ee Bwana.
5. Uwajalie marehemu wetu kuuona ufalme wako ukiwajia
kadiri ya huruma na upendo wako. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Mwanao Mpenzi, Yesu
Kristo, Bwana wetu. Amina.