IJUMAA JUMA 7 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO: Ybs.6:5–17
Maneno matamu yatamzidishia mtu rafiki, na midomo yenye neema itamwongezea wamsalimuo. Wale wenye
Amani nawe na wawe wengi; bali washauri wako mmoja katika elfu. Ukitaka kujipatia rafiki,
umpate kwa kumjaribu, wala usiwe na haraka katika kumwamini; yaani, kuna rafiki wakati wa kufaa,
ambaye yeye hatadumu wakati wa msiba wako. Tena kuna rafiki ageukaye kuwa adui, naye atakukashifia
fitina iletayo lawama. Pia kuna rafiki tena, ambaye anakula mezani pako, bali siku ya mabaya haonekani;
wakati wa kufanikiwa kwako atakuwa sawa nawe, na kupiga domo juu ya watumishi wako; lakini ukipatwa
na masaibu atakugeuka, na kujificha mbali nawe na uso wako. Basi ujitenge na adui zako; tena ujihadhari
na rafiki zako. Walakini rafiki aliye amini ndiye ngome; naye aliyempata amepata tunu. Hakuna badala
ya rafiki amini, wala uzuri wake hauna bei. Rafiki amini ni kifunga uzima; naye amchaye Mungu atampata.
Mcha Mungu hunyosha urafiki wake, kwa maana alivyo yeye mwenyewe ndivyo alivyo na jirani yake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:12,16,18,27,34–35. (K)35
1. Ee Bwana, umehimidiwa,
Unifundishe amri zako.
Nitajifurahisha sana kwa amri zako,
Sitalisahau neno lako.
(K) Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Ee Bwana.
2. Unifumbue macho yangu niyatazame,
Maajabu yatokayo katika sheria yako.
Unifahamishe njia ya mausia yako,
Nami nitayatafakari maajabu yako. (K)
3. Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.
Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako,
Kwa maana nimependezwa nayo. (K)
SHANGILIO: Zab.130:5
Aleluya, aleluya!
Roho yangu inamngoja Bwana,
na neno lake nimelitumainia.
Aleluya!
INJILI: Mk.10:1-12
Yesu alifika mipakani mwa Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani; makutano mengi wakakutanika tena
wakamwendea; akawafundisha tena kama alivyozoea. Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza,
Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu. Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru
nini? Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha. Yesu akawaambia, Kwa
sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu,
aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe;
na hao wawili watakuwa mwili mmoja, hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi
alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe. Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza
habari ya neno hilo. Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake;
na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Yesu Kristo ni rafiki yetu wa kweli, kwani
ametoa hata uhai wake kwa ajili yetu sisi wakosefu.
Basi, tumwombe.
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Umjalie Askofu wetu F. na mapadre wake wote
amani na furaha kwa kuyaona matunda ya kazi zao
za kichungaji wanazozifanya kila siku. Ee Bwana.
2. Uwaepushe wanadamu na kiburi au tamaa mbaya
ili wasidiriki kuyatangua maagano ambayo Wewe
unapenda yadumu milele. Ee Bwana.
3. Utujalie hekima ya kuwapata marafiki wa kweli, na
utuepushe na hila za yule mwovu. Ee Bwana.
4. Utupe ari ya kuwaiga manabii walionena kwa jina
lako, wawe mfano wa uvumilivu na wa kustahimili
mabaya; na utuepushe na viapo visivyofaa. Ee Bwana.
5. Uwarehemu marehemu wetu na kuwapa uzima wa
milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Bwana Yesu uliyetufundisha kuzishika kiaminifu
amri za Mungu, uyapokee maombi yetu. Unayeishi na
kutawala daima na milele. Amina.