JUMAMOSI JUMA 1 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: Isa30:19-21,23-26
Bwana Mungu Mtakatifu wa Israeli asema: Kwa maana watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe
hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu.
Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila
macho yako yatawaona waalimu wako; na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii,
ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto. Naye atatoa mvua juu ya
mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku
hiyo ng'ombe zako watakula katika malisho mapana. Ng'ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula
kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo. Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima
kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara. Na
tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba,
katika siku ile Bwana atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.147:1-6
1. Aleluya.
Msifuni Bwana; Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu,
Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri.
Bwana ndiye aijengaye Yerusalemu,
Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli. (K)
(K) Heri wote wamngojeao Bwana.
2. Huwaponya waliopondeka moyo,
Na kuziganga jeraha zao.
Huihesabu idadi ya nyota,
Huzipa zote majina. (K)
3. Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu,
Akili zake hazina mpaka.
Bwana huwategemeza wenye upole,
Huwaangusha chini wenye jeuri. (K)
Shangilio: Isa.33:22
Aleluya, aleluya.
Bwana ndiye mwamuzi wetu; Bwana ndiye mfanya sheria wetu; Bwana ndiye mfalme wetu; Ndiye atakayetuokoa.
Aleluya.
INJILI: Mt.9:35-10:1,6-8
Siku ile: Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri
habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia,
kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi
wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi
katika mavuno yake. Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na
kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba
ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa,
fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu zangu, ni kweli kwamba mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache. Basi, na tumwombe Bwana
wa mavuno tukisema:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umuimarishe Askofu wetu F. katika imani na mapendo na utuongezee watenda
kazi shambani mwako, ili wauhubiri ujio wa Mwanao duniani kote.
2. Wachungaji wetu wadumu katika kumhubiri Mkombozi, wala wasiliache Kanisa lako libaki kama
kondoo wasio na mchungaji.
3. Wakristo wawajue wachungaji wao, wachukuliane nao na kushirikishana malisho yaliyo mema daima.
4. Umjalie kila mmoja wetu kuwa nuru ya ulimwengu na utuponye mapigo ya majeraha yetu.
Ee Bwana, tunakuletea haya yote kwa kuwa wewe ni Mungu mwenye rehema nyingi, tena mwenye kutujibu
usikiapo kilio chetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.