JUMAMOSI JUMA 1 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Ebr.4:12-16
Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu. Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.19:7-9,14 (K) Yn.6:63
1. Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima.

(K) Wewe, Ee Bwana unayo maneno ya uzima wa milele.

2. Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru. (K)

3. Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa. (K)

4. Maneno ya kinywa changu,
Na mawazo ya moyo wangu,
Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana,
Mwamba wangu, na mwokozi wangu. (K)

SHANGILIO: Lk.4:18–19
Aleluya, aleluya,
Bwana amenituma kuwahubiri maskini habari njema,
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao.
Aleluya.

INJILI: Mk.2:13-17
Yesu alitoka, akaenda kando ya bahari, mkutano wote ukamwendea, akawafundisha. Hata alipokuwa akipita, akamwona Lawi wa Alfayo, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaondoka akamfuata. Hata alipokuwa ameketi chakulani nyumbani mwake, watoza ushuru wengi wa wenye dhambi waliketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwa maana walikuwa wengi wakimfuata. Na waandishi na Mafarisayo walipomwona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Bwana Mungu, neno lako li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Kwa maombezi ya Mama Bikira Maria, twakuomba:-

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Uwajalie makuhani na wote wenye Daraja Takatifu roho ya Mwanao Yesu Kristo, wapate kuchukuliana na watu wao katika maisha yao ya kila siku. Ee Bwana.

2. Viongozi wetu wa serikali, wa vyama vya siasa na wa taasisi mbalimbali watimize ahadi zao za kuleta haki, amani na usawa kwa watu wako. Ee Bwana.

3. Kwa maombezi ya Mama Bikira Maria, uwajalie wote waliopakwa mafuta kwa Ubatizo wafuate mfano wake wa unyenyekevu na kuwa wafuasi waaminifu wa Mwanao Yesu Kristo. Ee Bwana.

4. Utupe sisi sote ujasiri wa kushinda majaribu kama Mwanao Yesu Kristo alivyotufundisha kwa vitendo. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu F. wapewe rehema yako na kukaribishwa kwenye kiti chako cha neema. Ee Bwana.

Ee Mungu, Wewe watupatia neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. Utujalie hayo tuliyokuomba. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.