JUMAMOSI JUMA 22 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: 1Kor.4:6-15
Ndugu zangu, mambo hayo nimeyafanya kuwa mfano wa mimi na Apolo kwa ajili yenu, ili kwamba
kwa mfano wetu mpate kujifunza kutokupita yale yaliyoandikwa; ili mmoja wenu asijivune kwa
ajili ya huyu, kinyume cha mwenziwe. Maana ni nani anayekupambanua na mwingine? Nawe una nini
usichokipokea? Lakini iwapo ulipokea, wajisifia nini kana kwamba hukupokea? Mmekwisha kushiba,
mmekwisha kupata utajiri, mmemiliki pasipo sisi. Naam, laiti mngemiliki, ili sisi nasi tumiliki
pamoja nanyi! Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa
wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu. Sisi tu wapumbavu kwa
ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna
nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima. Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu,
tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao; kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu
wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama
takataka za dunia, na tamaa ya vitu vyote hata sasa. Siyaandiki hayo ili kuwatahayarisha; bali
kuwaonya kama watoto niwapendao. Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini
hamna baba wengi. Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.145:17-21(K)18
1. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana yu karibu na wote wamwitao,
Wote wamwitao kwa uaminifu.
(K) Bwana yu karibu na wote wamwitao.
2. Atawafanyia wamchao matakwa yao,
Naye atakisikia kilio chao na kuwaokoa.
Bwana huwahifadhi wote wampendao,
Na wote wasio haki atawaangamiza. (K)
3. Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana;
Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu milele na milele. (K)
SHANGILIO: Yn.14:6
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya!
INJILI: Lk.6:1-5
Ilikuwa siku ya sabato moja alikuwa akipita katika mashamba, wanafunzi wake wakawa wakivunja
masuke na kuyala, wakiyapukusa-pukusa mikononi mwao. Basi baadhi ya Mafarisayo wakawaambia,
Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato? Yesu akawajibu akawaambia, Hamkulisoma hata hilo
alilolifanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale aliokuwa nao? Jinsi alivyoingia katika
nyumba ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya Wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe, ambayo si
halali kuila ila kwa makuhani peke yao. Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, tumwombe Mungu kwa maombezi ya Bikira
Maria mama yetu tukisema:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Askofu wetu F. na Mapadre wote wadumu katika
kulihubiri neno lako na kuumega mkate, ili watu
wako wapate daima kushibishwa kwa mema yako. Ee Bwana.
2. Viongozi wetu wa serikali wawapiganie wanaowahudumia
watu wako katika mazingira magumu,
ili wapate unafuu wa maisha. Ee Bwana.
3. Uingilie kati vita na dhuluma vilivyo dhidi ya watu
wasio na hatia, ili amani itawale na waamini wako
wakuabudu kwa utulivu. Ee Bwana.
4. Uwajalie wakristo wote kuikiri imani kwa imara ya
kudumu, wakifuata mashauri ya Injili yenye tumaini
la kweli. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wajaliwe amani isiyo na kikomo
huko juu mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetupatanisha ili tuwe watakatifu bila
mawaa, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.