JUMAMOSI JUMA 25 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Mhu.11:9-12:8
Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee
njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo
yote Mungu atakuleta hukumuni. Kwa hiyo ondoa majonzi moyoni mwako, nawe uuondoe ubaya mwilini
mwako; kwa maana ujana ni ubatili, na utu uzima pia. Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako,
Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika
hiyo. Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya
mvua; Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema; Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; Na wasagao
kukoma kwa kuwa ni haba; Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza; Na milango kufungwa katika
njia kuu; Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; Na mtu kusituka kwa sauti ya ndege; Nao binti za
kuimba watapunguzwa; Naam, wataogopa kilichoinuka Na vitisho vitakuwapo njiani; Na mlozi
utachanua maua; Na panzi atakuwa ni mzigo mzito; Na pilipili hoho itapasuka; Maana mtu aiendea
nyumba yake ya milele, Nao waombolezao wazunguka njiani. Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au
kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani; Nayo
mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa. Mhubiri asema,
Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!
WIMBO WA KATIKATI: Zab.90:3-6,12-14,17(K)1
1. Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo,
Rudini, enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako
Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kesha la usiku.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi.
2. Wawagharikisha, huwa kama usingizi,
Asubuhi huwa kama majani yameayo.
Asubuhi yachipuka na kumea,
Jioni yakatika na kukauka. (K)
3. Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee Bwana urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako. (K)
4. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti,
Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe. (K)
SHANGILIO: 2Tim.1:10
Aleluya, aleluya!
Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika,
kwa ile Injili;
Aleluya!
INJILI: Lk.9:43-45
Makutano walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake,
Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono
ya watu. Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza
maana yake neno lile.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu alipenda kumtukuza Mwanae Yesu Kristo
hapa duniani kwa namna mbali mbali. Pamoja na
Bikira Maria, tumpelekee Mungu maombi yetu:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Umwongezee Baba Mtakatifu F. na viongozi wote
wa Kanisa ujasiri katika kuyatetea mafumbo makuu
ya imani yetu wakati wote na katika mazingira yoyote. Ee Bwana.
2. Ulikinge Kanisa lako na hila za wanaompinga Kristo
wako, tupate kuepukana na maasi na kuuona utukufu
wa Mwanao kati yetu. Ee Bwana.
3. Utuongezee imani juu ya uwepo wako kati yetu
katika neno lako, katika Sakramenti na katika
wenzetu; na utuondolee hofu na mahangaiko. Ee Bwana.
4. Vijana wote wakukumbuke Wewe muumba wao
wakati bado wanaufurahia ujana wao; ili matendo
yao mema yakubalike siku ya hukumu. Ee Bwana.
5. Uwaite ndugu zetu marehemu wapate kuishi pamoja
nawe milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.