JUMAMOSI JUMA 26 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Ayu.42:1-3,5-6,12-17
Ayubu alimjibu Bwana na kusema, najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, na yakuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika. Ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa? Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, mambo ya ajabu, ya kunishinda mimi, nisiyoyajua. Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; bali sasa jicho langu linakuona. Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu katika mavumbi na majivu. Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng’ombe elfu, na punda wake elfu. Tena alikuwa na wana waume saba, na binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu. Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume. Kisha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia na arobaini, naye akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hata vizazi vine. Basi Ayubu akafa, mzee sana mwenye kujawa na siku.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:66,71,75,91,125,130(K)135
1. Unifundishe akili na maarifa,
Maana nimeyaamini maagizo yako.
Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa,
Nipate kujifunza mari zako.

(K) Umwangazie mtumishi wako uso wako, Ee Bwana.

2. Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki,
Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa.
Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo,
Maana vitu vyote ni watumishi wako. (K)

3. Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe,
Nipate kuzijua shuhuda zako.
Kufananisha maneno yako kwatia nuru,
Na kumfahamisha mjinga. (K)

SHANGILIO: Yn.15:15
Aleluya, aleluya!
Bwana anasema: Siwaiti tena watumwa, lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu, nimewaarifu.
Aleluya!

INJILI: Lk.10:17-24
Wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni. Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Akawageukia wanafunzi wake, akasema nao kwa faragha, Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi. Kwa kuwa nawaambia ya kwamba manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi wasiyasikie.