JUMAMOSI JUMA 27 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Gal.3:22-29
Andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa
Imani ya Yesu Kristo. Lakini kabla ya kuja ile Imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa
mpaka ije ile Imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe
haki kwa Imani. Lakini, iwapo Imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote
mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya Imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika
Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala
mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi,
mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:2-7(K)8
1. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.
2. Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake siku zote.
Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya,
Miujiza yake na hukumu za kinywa chake. (K)
3. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake,
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake. (K)
SHANGILIO: Zab.119:18
Aleluya, aleluya!
Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya!
INJILI: Lk.11:27-28
Ikawa, Yesu alipokuwa akisema, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia
Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya. Lakini yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao
neno la Mungu na kulishika.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Mungu ni kimbilio letu na ngome yetu.
Walisikiao neno lake na kulishika ndio wenye heri.
Tumwombe Mungu kupitia Mama yetu Bikira Maria.
tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Askofu wetu F. na Mapadre wetu wote wazidi kuwa
madhubuti kimwili na kiroho, wapate kuwaimarisha
watu wao katika imani na mapendo kwako. Ee Bwana.
2. Uwe pamoja na viongozi wetu wa serikali
wanaolisikia neno lako na kulishika; na uwahesabie
haki kwa imani, wapate kuwa warithi sawasawa na
ahadi yako kwa wakuaminio. Ee Bwana.
3. Watu wote duniani wajaliwe kujiandaa kwa ajili ya
siku yako ya hukumu ambayo unaifahamu Wewe tu. Ee Bwana.
4. Uwabariki wazazi wetu na utujalie kuutetea uhai
wetu na wa wenzetu, wakubwa kwa wadogo, kama
neno lako linavyotuamuru. Ee Bwana.
5. Uwahurumie ndugu zetu marehemu na kuwapa furaha
isiyo na mwisho huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, uliyependa Bikira Maria apewe heri kufuatia
matendo makuu ya Mwanao, uyapokee maombi yetu.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.