JUMAMOSI JUMA 28 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO Efe 1:15-23
Tangu nilipopata habari za Imani yenu katika bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote, siachi
kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu, Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo,
Baba wa utukufu awape ninyi roho wa hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu
yatiwe nuru, tumjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo ;na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika
watakatifu jinsi ulivyo. Kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake;ulipotenda katika kristo
alipomfufua katika wafu,akamwekea mkono wake wa kuume katika ulimwngu wa roho ; juu sana katika
ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani na kila jina litajwalo wala si ulimwenguni humu tu
bali katika ule ujao pia akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu
vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika
vyote.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.8:1-6
1. Wewe Mungu Bwana wetu,
Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni;
Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao.
(K) Umemtawaza mwanao juu ya kazi za mikono yako
2. Nikiziangalia mbingu zako, Kazi ya vidole vyako,
Mwezi na nyota ulizoziratibisha,
Mtu ni kitu gani hat umkumbuke
Na binadamu hata umwangalie. (K)
3. Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima
Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako
Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake. (K)
SHANGILIO: Yn.14:5
Aleluya, aleluya!
Nakushukuru baba Bwana wa mbingu na nchi, Kwa kuwa mambo haya uliyaficha
Wenye hekima na akili, Ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya!
INJILI: Lk.12:8-12
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa
Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu; na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo
atakanwa mbele ya malaika wa Mungu. Na kila mtu atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa,
bali aliyemkufura Roho Mtakatifu hatasamehewa. Na watakapowapeleka ninyi mbele ya masinagogi na
maliwali na wenye mamlaka, msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema; kwa
kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, Mwanao Yesu Kristo ametuasa tumkiri yeye
mbele ya watu na ametuangalisha dhidi ya kumkufuru
Roho wako Mtakatifu. Tunahitaji neema yako. Kwa
maombezi ya Bikira Maria, utujalie:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na wote wanaolichunga
kundi lako wawafikishie Injili yako waamini
wote, ili nao wapate kukujua zaidi Wewe. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia wasifadhaishwe na imani yetu
juu ya Kristo Mfufuka; bali wamkiri kuwa yu juu
ya vitu vyote. Ee Bwana.
3. Uifungue mioyo ya wote wasiolikiri jina lako
wapate kuongoka na kujiandaa vema kwa ujio wa
Mwanao Yesu Kristo siku ya mwisho. Ee Bwana.
4. Roho wako Mtakatifu atufundishe daima tunayopaswa
kuyasema mbele ya wapinzani au watesi wetu
tupate kukukiri Wewe kwa ujasiri na ufasaha wote.
Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wahesabiwe haki ya kuirithi
mbingu, kwa kadiri ya huruma yako. Ee Bwana.
Ee Mungu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.