JUMAMOSI JUMA 2 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: Ybs.48:1-4,9-11
Ndipo aliposimama nabii Eliya, kama moto, hata na neno lake likawaka kama tanuru. Yeye alileta njaa
juu yao, na kwa juhudi yake akawapunguzia hesabu yao; kwa neno la Bwana akazifunga mbingu, na mara
tatu kutoka huko akatelemsha moto. Jinsi ulivyotisha kwa miujiza yako! Aliye mfano wako ataona fahari.
Akachukuliwa juu katika kisulisuli, katika gari la farasi wa moto. Ukaandikiwa kuwa utaleta makemeo, ili
kutuliza hasira siku ile ya Bwana; kugeuza moyo wa baba umwelekee mwana na kuhuisha kabila za Israeli.
Bila shaka wamebarikiwa wale waliokuona kwa macho, wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana
unaishi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.80:1-2,14-15,17-18
1. Wewe uchungaye Israeli, usikie,
Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.
Uziamshe nguvu zako. (K)
(K) Ee Bwana Mungu wetu, uturudishe, Utuangazishe uso wako, nasi tutaokoka.
2. Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,
Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.
Na mche ule ulioupanda Kwa mkono wako wa kuume;
Na tawi lile ulilolifanya Kuwa imara kwa nafsi yako. (K)
3. Mkono wako na uwe juu yake Mtu wa mkono wako wa kuume;
Juu ya mwanadamu uliyemfanya Kuwa imara kwa nafsi yako;
Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma;
Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako. (K)
Shangilio: Lk.3:4,6
Aleluya, aleluya,
Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake,
Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu,
Aleluya.
INJILI: Mt.17:10-13
Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani: Wanafunzi wake wakamwuliza, wakisema, Basi kwa nini waandishi hunena
ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza? Naye akajibu, akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza, naye atatengeneza
yote, ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo
hivyo Mwana wa Adamu naye yuaenda kuteswa kwao. Ndipo wale wanafunzi walipofahamu ya kuwa amesema nao habari
za Yohane Mbatizaji.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Bwana, sisi tumezidi kubarikiwa, kwa maana tunaishi huku tukiwa na fursa ya kujikumbusha matakwa yako.
Basi twakuomba:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Upokee shukrani yetu kwa kuwa upendo wako kwetu hauna mipaka na umuimarishie Askofu
wetu F. afya ya mwili na roho. Ee Bwana.
2. Utuongoze nyakati zote hata pale tunaposhindwa kuyatambua na kuyatimiza mapendo yako kwetu. Ee Bwana.
3. Maumivu ya moto yatukumbushe ukali wa adhabu yako kwa wakosefu wasiotaka kutubu, kusudi tupate nguvu ya
kutubu mara tukukoseapo wewe au jirani zetu. Ee Bwana.
4. Utuepushe na laana ya kutowajali na hata kuwatenda vibaya wajumbe wako unaowatuma kwetu. Ee Bwana.
Ee Mungu, Mwanao aliteswa kwa sababu ya dhambi zetu. Utujalie ujio wake wa pili uwe kipatanisho cha dhambi
zetu. Kwa huyo Kristo Bwana wetu. Amina.