JUMAMOSI JUMA 32 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: 3Yoh.1:5-8
Mpenzi, kazi ile ni ya uaminifu uwatendeayo hao ndugu na hao wageni nao, waliokushuhudia upendo
wako mbele ya kanisa; utafanya vizuri ukiwasafirisha kama ipasavyo kwa Mungu. Kwa maana, kwa ajili
ya Jina hilo, walitoka, wasipokee kitu kwa Mataifa. Basi imetupasa sisi kuwakaribisha watu kama hao,
ili tuwe watenda kazi pamoja na kweli.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.112:1-6(K)1
Aleluya.
1. Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo yake
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
(K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
2. Nyumbani mwake mna utajiri na mali,
Na haki yake yakaa milele.
Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki. (K)
3. Heri atendaye fadhili na kukopesha;
Atengenezaye mambo yake kwa haki.
Kwa maana hataondoshwa kamwe;
Mwenye haki atakumbukwa milele. (K)
SHANGILIO: Zab.130:5
Aleluya, aleluya!
Roho yangu inamngoja Bwana, na neno lake nimelitumainia.
Aleluya!
INJILI: Lk.18:1-8
Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate
tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji Fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika
mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui
wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali
watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia
daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule
wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini,
atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona Imani duniani?
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu aliyewakomboa Waisraeli utumwani
Misri kwa mkono wa Musa, ndiye aliyetukomboa sisi
toka utumwa wa dhambi kwa njia ya Mwanae Yesu
Kristo. Kwa maombezi ya Bikira Maria, tumwombe.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Ubariki juhudi za Maaskofu na Wakleri wote katika
kuhubiri toba iletayo msamaha wa dhambi kwa watu
wako. Ee Bwana.
2. Uwe pamoja na viongozi wetu wa serikali ili, hata
wafanyapo mikataba na watu wa mataifa mengine,
wazilinde mila na desturi zetu njema; tupate kuwa
watenda kazi pamoja na kweli. Ee Bwana.
3. Matukio ya kihistoria yanayoonesha nguvu yako kuu
dhidi ya yule mwovu na upendo wako mkuu kwa watu
wako, yawe kichocheo cha wongofu wa watu
wengi. Ee Bwana.
4. Utuongezee ari ya kusali bila kuchoka na udumifu
katika kutenda mema tukisukumwa na upendo kwako
na kwa wenzetu. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wasamehewe dhambi zao na
kufikishwa huko uliko Wewe. Ee Bwana.
Ee Mungu unayewapatia haki wanaokulilia, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.