JUMAMOSI JUMA 33 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Ufu.11:4-12
Mimi, Yohane, nilisikia sauti isemayo: Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi. Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka katika vinywa vyao na kuwala adui zao. Na mtu akitaka kuwadhuru, hivyo ndivyo impasavyo kuuawa. Hao wana amri ya kuzifunga mbingu, ili mvua isinye katika siku za unabii wao. Na wana amri juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuipiga nchi kwa kila pigo, kila watakapo. Hata watakapoumaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua. Na mizoga yao itakuwa katika njia ya mji ule mkuu, uitwao kwa jinsi ya roho Sodoma, na Misri, tena ni hapo Bwana wao aliposulibiwa. Na watu wa hao jamaa na kabila na lugha na taifa waitazama mizoga yao siku tatu u nusu, wala hawaiachi mizoga yao kuwekwa kaburini. Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi. Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama. Wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.144:1-2,9-10(K)1
1. Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu,
Anifundishaye mikono yangu vita,
Vidole vyangu kupigana.

(K) Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu.

2. Mhisani wangu na boma langu,
Ngome yangu na mwokozi wangu,
Ngao yangu niliyemkimbilia,
Huwatiisha watu wangu chini yangu. (K)

3. Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya,
Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia.
Awapaye wafalme wokovu,
Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu. (K)

SHANGILIO: Yn.14:5
Aleluya, aleluya!
Neno la Kristo likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.
Aleluya!

INJILI: Lk.20:27-40
Baadhi ya masadukayo, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, walimwendea Yesu, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto, na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; na wa pili akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto; hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. Mwisho akafa yule mke naye. Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionesha katika sura ya Kijiti, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake. Waandishi wengine wakajibu wakamwambia, Mwalimu, umesema vema; wala hawakuthubutu kumwuliza neno baada ya hayo.