JUMAMOSI JUMA 3 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.11:1–2,8–19
Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Maana kwa hiyo
wazee wetu walishuhudiwa. Kwa Imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopata
kuwa urithi; akatoka asijue aendako. Kwa Imani alikaa nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na
Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi,
ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu. Kwa Imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba,
alipokuwa amepita wakati wake, kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu. Na kwa ajili ya
hayo wakazaliwa na mtu mmoja, naye alikuwa kama mfu, watu wengi kama nyota za mbinguni wingi wao, na
kama mchanga ulio ufuoni, usioweza kuhesabika. Hawa wote wakafa katika Imani, wasijazipokea zile
ahadi bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri
juu ya nchi. Maana hao wasemao maneno kama hayo waonesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe.
Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafsi ya kurejea. Lakini sasa waitamani nchi
iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji.
Kwa Imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa
akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee; Naam, yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya
kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano.
WIMBO WA KATIKATI: Lk.1:69–75 (K)68
1. Ametusimamishia pembe ya wokovu
Katika mlango wa Daudi mtumishi wake.
Kama alivyosema tangu mwanzo
Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu.
(K) Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,
kwa kuwa amewajia watu wake.
2. Tuokolewe na adui zetu
Na mikononi mwao wote wanaotuchukia:
Ili kuwatendea rehema baba zetu,
Na kulikumbuka agano lake takatifu. (K)
3. Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu,
Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu,
Na kumwabudu pasipo hofu
Kwa utakatifu na kwa haki
Mbele zake siku zetu zote. (K)
SHANGILIO: Yn.14:23
Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu,
na baba yangu atampenda,
na sisi tutakuja kwake.
Aleluya.
INJILI: Mk.4:35-41
Siku ile kulipokuwa jioni, Yesu akawambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua
vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya
upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri,
amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka,
akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia,
Mbona mmekuwa waoga? Hamna Imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata
upepo na bahari humtii?
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, kwa maombezi ya Bikira Maria tunakuletea
maombi yetu tukisema.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa
wazidi kuilinda imani na kuifundisha kwa watu wako.
Ee Bwana.
2. Wote wenye dhamana ya uongozi wawalinde watu
wao dhidi ya dhoruba za maisha, ili walifikie
salama lengo lao la kuwepo hapa duniani. Ee
Bwana.
3. Utujalie sisi sote tamaa ya nchi iliyo bora zaidi, yaani
ya mbinguni. Ee Bwana.
4. Kwa maombezi ya Bikira Maria, utujalie toba ya kweli kwa dhambi zetu na msamaha
kwa waliotukosea. Ee Bwana.
5. Uwapokee marehemu wetu katika amani yako huko mbinguni. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Mwanao mpenzi, Yesu
Kristo. Amina.