JUMAMOSI JUMA 4 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Ebr.13:15-17,20-21
Kwa njia yake Yesu, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake. Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu. Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi. Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu, awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, mpate kuyafanya mapenzi yake, naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake, kwa Yesu Kristo; utukufu una yeye milele na milele. Amina.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.23:1-6. (K)1
1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
Hunihuisha nafsi yangu;

(K) Bwana ndiye mchungaji wangu sitapungukiwa na kitu.

2. Huniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)

3. Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K)

4. Hakika wema na fadhili zitanifuata
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

SHANGILIO: Zab.119:105
Aleluya, aleluya,
Neno lako ni taa ya kuniongoza,
na mwanga katika njia yangu.
Aleluya.

INJILI: Mk.6:30-34
Mitume walikusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha. Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha; mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwako nafasi ya kula. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu. Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika. Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.

--------------

--------------
MAOMBI
Kupitia Mama yetu Bikira Maria, tumpelekee Mungu maombi yetu kwa niaba ya Kanisa zima:-

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na wote wenye Daraja Takatifu wadumu katika kuliongoza kundi lako, ili lisibaki kama kondoo wasio na mchungaji. Ee Bwana.

2. Viongozi wetu wa kijamii wajaliwe utawala bora na hivi kushirikiana na watu wao katika kutenda yakupendezayo Wewe. Ee Bwana.

3. Kila mmoja wetu akirimiwe utii na unyenyekevu kwa wanaotuongoza na hata kukesha kwa ajili yetu kwa moyo mnyofu. Ee Bwana.

4. Umjalie kila mwanajamii kutumia busara aliyopewa nawe katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha; ili kudumisha haki, amani na usawa. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wapokelewe katika kundi lako la watakatifu huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Bwana, utujalie hayo ili yatufae kwa wokovu ule alioupata Bikira Maria na watakatifu wote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.