JUMAMOSI JUMA 7 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO: YbS.17:1–15
Bwana alimwumba Adamu katika mavumbi, na hata mavumbini akamrudisha. Akawapa wanadamu siku kwa idadi,
na mihula iliyoamriwa; akawapa amri juu ya vitu vilivyomo; akawavika nguvu kama Yeye mwenyewe, na
kuwafanya kwa mfano wake. Akaitia hofu ya binadamu katika vyote vyenye mwili, ili wawatawale wanyama
na ndege. Akawajaza maarifa ya hekima, na kuwapa kupambanua wema na uovu. Akawafanyizia ulimi, na
macho, na masikio, akawapa na moyo wa ufahamu. Ili kuwaonesha adhama ya kazi yake, ili wajisifie
katika miujiza yake, na kukijulisha kicho chake ulimwenguni, na kulihimidi jina lake takatifu;
aliyaweka mbele yao maarifa, akawapa sheria ya uzima kuwa urithi. Alifanya na wateule wake agano
la milele, na kuwaonesha hukumu zake. Kwa macho yao waliiona enzi ya utukufu wake, na kwa masikio
yao waliisikia sauti yake yenye nguvu. Akawaambia, Jihadharini na yasiyo haki, akawapa amri kila
mtu juu ya jirani yake. Njia zao nazo zi mbele zake daima, wala hazitafichwa machoni pake.
WIMBO WA KATIKATI: zab.103:13-18(K)17
1. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake,
Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.
Kwa maana Yeye anatujua umbo letu,
Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.
(K) Fadhili za Bwana zina wamchao tangu milele hata milele.
2. Mwanadamu siku zake zi kama majani;
Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo.
Maana upepo hupita juu yake, kumbe haliko!
Na mahali pake hapatalijua tena. (K)
3. Bali fadhili za Bwana zina wamchao Tangu milele hata milele,
Na haki yake ina wana wa wana;
Maana, wale walishikao agano lake,
Na kuyakumbuka maagizo yake ili wayafanye. (K)
SHANGILIO: Zab.130:5
Aleluya, aleluya!
Roho yangu inamngoja Bwana,
na neno lake nimelitumainia.
Aleluya!
INJILI: Mk.10:13-16
Makutano walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona
alichukuzwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama
hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo
hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, uliyemwumba mwanadamu kwa sura na
mfano wako na kumpa amri juu ya vitu vyote duniani,
twakuomba.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie viongozi wanaolihudumia Kanisa badala
ya Mwanao, Yesu Kristo, kuonesha adhama ya kazi
yake na kulihimidi jina lake takatifu. Ee Bwana.
2. Wote uliowajaza hekima na maarifa ya dunia hii
wajaliwe kuvitumia vipaji hivyo kwa sifa na utukufu
wako na kukijulisha kicho chako ulimwenguni. Ee Bwana.
3. Uwajalie wabatizwa wote kuiona enzi ya utukufu
wako, kuisikia sauti yako yenye nguvu na kumtendea
haki jirani. Ee Bwana.
4. Utuongezee moyo wa sala; na uwaimarishie
wagonjwa imani katika uwezo wako wa kuponya
roho na mwili kwa Sakramenti ya Mpako
Mtakatifu. Ee Bwana.
5. Kwa maombezi ya Mama Bikira Maria, marehemu
wetu wafikishwe mbele ya uso wako mtukufu. Ee
Bwana.
Ee Baba mwema unayetaka tuukubali ufalme wako kama
watoto wadogo, upokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.