JUMANNE JUMA 1 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.2:5-12
Mungu hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali fulani,
akisema, Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko
malaika, Umemvika taji ya utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umeweka vitu vyote chini ya
nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado
hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake. ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu,
kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili
ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana
wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye atakasaye na hao
wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake; akisema, Nitalihubiri jina
lako kwa ndugu zangu; Katikati ya kanisa nitakuimbia sifa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.8:2,5-9 (K)7
1. Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao Umeiweka misingi ya nguvu;
Kwa sababu yao wanaoshindana nawe;
Uwakomeshe adui na mijilipiza kisasi.
Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
(K) Umemtawaza mwanao juu ya kazi ya mikono yako.
2. Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako;
Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake.
Kondoo, na ng'ombe wote pia;
Naam, na wanyama wa kondeni; (K)
3. Ndege wa angani, na samaki wa baharini;
Na kila kipitacho njia za baharini.
Wewe, MUNGU, Bwana wetu, Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! (K)
SHANGILIO: Ebr.4:12
Aleluya, aleluya,
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu,
li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya.
INJILI: Mk.1:21-28
Yesu na wanafunzi wake walishika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi,
akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri,
wala si kama waandishi. Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti,
akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa
Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti
kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza
awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando
ya Galilaya.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, sisi wanadamu tumefanywa wadogo punde
kuliko malaika na tumevikwa taji ya utukufu na heshima.
Tumwombe Mungu tukisema.
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Viongozi wote wa dini na wa serikali wawakumbuke
na kuwajali watu wote walio chini yao. Ee Bwana.
2. Sisi sote tuige mfano wa Mwanao Yesu Kristo,
wa kuwa tayari kupata maumivu na hata mauti kwa
ajili ya upendo kwa wenzetu. Ee Bwana.
3. Kila mmoja wetu amtii malaika wake mlinzi katika
maongozi yake. Ee Bwana.
4. Utuimarishie imani, moyo wa sala na ari ya kutimiza
nadhiri zetu kwako. Ee Bwana.
5. Malaika wako wawafikishe kwako mbinguni ndugu
zetu marehemu. Ee Bwana.
Ee Mungu mwenye nguvu, uyasikilize maombi yetu. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.