JUMANNE JUMA 22 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: 1Kor.2:10-16
Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya
binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake?
Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea
roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.
Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa
na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanadamu wa tabia ya asili
hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa
yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni kuyatambua yote, wala yeye hatambuliwi
na mtu. Maana, ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.145:8-14(K)17
1. Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
(K) Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote.
2. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako.
Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
Na utukufu wa fahari ya ufalme wake. (K).
3. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinama chini. (K)
SHANGILIO: Ebr.4:12
Aleluya, aleluya!
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu, li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya!
INJILI: Lk.4:31-37
Yesu alishuka mpaka Kapernaumu, mji wa Galilaya, akawa akiwafundisha siku ya sabato; wakashangaa
mno kwa mafundisho yake, kwa kuwa neno lake lilikuwa na uwezo. Na ndani ya sinagogi mlikuwa na
mtu mwenye roho ya pepo mchafu, akalia kwa sauti kuu, akisema, Acha! Tuna nini nawe, Yesu wa
Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema,
Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno. Mshangao
ukawashika wote, wakasemezana wakisema, Ni neno gani hili, maana awaamuru pepo wachafu kwa
uwezo na nguvu, nao hutoka. Habari zake zikaenea kila mahali katika nchi ile.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, malaika wanakutumikia daima huko
mbinguni. Kwa vile nasi twatamani kufika huko
waliko, tunakuomba tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umjalie Askofu wetu F. na wahubiri wote wa neno
lako kuwakumbusha watu, kwamba siku yako
itakuja ghafla kama mwivi. Ee Bwana.
2. Ubariki juhudi za viongozi wetu wa serikali, ili kazi
zao njema zitufae sisi sote. Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote kujiandaa vema kwa ujio wako
Bwana siku ya mwisho ili, hata ukija ghafla, utukute
tukikesha katika nuru yako. Ee Bwana.
4. Roho wako anayeyachunguza yote, awajalie
wanaoutafuta ukweli kutambua kuwa yanayofundishwa
na Roho hufasiriwa kwa maneno ya rohoni. Ee Bwana.
5. Uwaponye wagonjwa wetu, uwafukuze pepo
wabaya, na uwajalie ndugu zetu marehemu
uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tukeshe na kuwa na kiasi, uipokee
sala yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.