JUMANNE JUMA 23 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: 1Kor.6:1-11
Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala
si mbele ya watakatifu? Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimengu? Na ikiwa ulimwengu
utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? Hamjui ya kuwa tutawahukumu
malaika, basi si Zaidi sana na mambo ya maisha haya? Basi, mkiwa na mahali panapohukumiwa mambo
ya maisha haya, mwawaweka kuwa waamuzi hao waliohesabiwa kuwa si kitu katika kanisa? Nasema
hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima,
awezaye kukata maneno ya ndugu zake? Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao
wasioamini. Basi imekuwa upungufu kwenu kabisa kwamba mnashitakiana ninyi kwa ninyi wenyewe
mwadhulumu watu na kunyang’anya mali zao; naam, hata za ndugu zenu. Au hamjui ya kuwa wadhalimu
hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,
wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi. Na baadhi yenu
mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika
jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.149:1-6,9(K)4
1. Aleluya.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
(K) Bwana awaridhia watu wake.
2. Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)
3. Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote.
Aleluya. (K)
SHANGILIO: Zab.111:7,8
Aleluya, aleluya!
Maagizo yako yote, Ee Bwana, ni amini, yamethibitika milele na milele.
Aleluya!
INJILI: Lk.6:12-19
Yesu aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata
kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao
aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohane,
na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote,
na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti. Akashuka pamoja nao, akasimama
mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi
wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao;
na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa. Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa,
kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Bwana wetu Yesu Kristo tuliyempokea
ametufanya hai na imara kwa imani. Tunamshukuru
pamoja na malaika watakatifu na kumwomba:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uwajalie Baba Mtakatifu F.,
Askofu wetu F. na
Mapadre wote ambao ni warithi wa kazi ya mitume
kuutimiza wajibu huo mkubwa, ili watu wakujue na
kukuongokea Wewe. Ee Bwana.
2. Viongozi wa serikali waunge mkono juhudi za
wahubiri wa neno lako kukemea dhuluma, wizi,
ulevi, unyang'anyi na madhambi yote. Ee Bwana.
3. Malaika wako wawalinde wafuasi wa Mwanao Yesu
Kristo dhidi ya mafundisho potofu, na wawaongoze
kunako ukweli. Ee Bwana.
4. Utujalie sisi sote kutekeleza wajibu wa kuwa mitume
miongoni mwetu, ili watu wapate kumjua Mwanao
Yesu Kristo na kusaidiwa katika matatizo yao. Ee
Bwana.
5. Uwaponye wenye kuonewa na ibilisi na uwape marehemu
wetu uzima wa milele mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetaka sala ituunganishe sisi na Wewe,
uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.