JUMANNE JUMA 24 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: 1Kor.12:12-14,27-31
Kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinywesha Roho mmoja. Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake. Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha. Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kupnya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri? Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonesha njia iliyo bora.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.100(K)3
1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba.

(K) Tu watu wake na kondoo wa malisho yake.

2. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake na kondoo wa malisho yake. (K)

3. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)

SHANGILIO: Lk.7:16
Aleluya, aleluya!
Nabii mkuu ametokea kwetu; na Mungu amewaangalia watu wake.
Aleluya!

INJILI: Lk.7:11-17
Yesu alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu Baba, malaika wanayalinda maisha yetu hapa duniani. Hata hivyo, Wewe wabaki kuwa Mkuu kuliko vitu vyote. Na hivyo twakuomba:-

Kiitikio: Upokee sala yetu.
1. Umjalie Askofu wetu F. kudumisha fadhila ya upendo wa kweli na uaminifu kwa Jimbo lake na kwa Kanisa kwa ujumla. Ee Bwana.

2. Tunawaombea viongozi wote, wapate kuheshimiana na kusaidiana; ili karama zao ziwe kwa manufaa ya watu wao. Ee Bwana.

3. Wote walio katika malezi, wajaliwe kujiandaa vema hatua kwa hatua; waijue vema miito yao na kuishika siri ya imani katika dhamiri safi. Ee Bwana.

4. Utujalie kumwendea Mwanao Yesu Kristo kwa imani na matumaini ya kusaidiwa katika matatizo yetu ya kimwili na kiroho. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wajaliwe kukujia Wewe kwenye ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetaka kila mmoja wetu atimize kiaminifu ahadi au viapo vya wito wake, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.