JUMANNE JUMA 25 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Mit.21:1-6,10-13
Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; kama mfereji wa maji huugeuza popote apendapo.
Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; bali Bwana huipima mioyo. Kutenda haki na
hukumu humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka. Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, hata
ukulima wa waovu, ni dhambi. Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; bali kila mwenye pupa
huuelekea uhitaji. Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo ni moshi upeperushwao; ni kutafuta
mauti. Nafsi ya mtu mbaya hutamani maovu; jirani yake hapati fadhili machoni pake. Mwenye mzaha
aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa. Mwenye haki
huitafakari nyumba ya mtu mbaya; jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia. Azibaye masikio yake
asisikie kilio cha maskini, yeye naye atalia, lakini hatasikiwa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:1,27,30,34-35,44(K)35
1. Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Unifahamishe njia ya mausia yako,
Nami nitayatafakari maajabu yako.
(K) Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Ee Bwana.
2. Nimeichagua njia ya uaminifu,
Na kuziweka hukumu zako mbele yangu.
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote. (K)
3. Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako,
Kwa maana nimependezwa nayo.
Nami nitaitii sheria yako daima,
Naam, milele na milele. (K)
SHANGILIO: 1Pet.1:25
Aleluya, aleluya!
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya!
INJILI: Lk.8:19-21
Walimwendea Yesu mama yake na ndugu zake, wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano. Akaletewa
habari akiambiwa, Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe. Akawajibu
akasema, Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tumwombe Mungu aliyetuita katika imani na
anayetawala maisha yetu tukisema:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Umjalie Askofu wetu F. na Wachungaji wote wa
Kanisa lako kuwaimarisha waamini wao, katika
kufundisha imani na kuadhimisha mafumbo ya
ukombozi. Ee Bwana.
2. Ubariki juhudi za wote wenye mamlaka,
wanaoshirikiana na Wachungaji wako, katika
kuifanikisha kazi ya ukombozi wa watu wako. Ee Bwana.
3. Tunakushukuru kwa zawadi ya imani uliyotujalia,
na tunaomba utusaidie kudumisha udugu na umoja
katika Kristo Mwanao. Ee Bwana.
4. Tunawaombea wajasiriamali wote, ili wasitafute
utajiri ila mahitaji; na akiba yao halali iwe fadhili
kwa jirani mwenye shida. Ee Bwana.
5. Uwakaribishe ndugu zetu marehemu kwenye makao
yako ya milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayependa tukae pamoja kama ndugu na
kulisikiliza neno lako, uyapokee maombi yetu. Kwa njia
ya Kristo Bwana wetu. Amina.