JUMANNE JUMA 27 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Gal.1:13-24
Mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa
la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi
walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba
zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake,
alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara
sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu; wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa
mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski. Kisha, baada ya
miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano.
Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana. Na hayo ninayowaandikia, angalieni,
mbele za Mungu, sisemi uongo. Baadaye nalikwenda pande za Shamu na Kilikia. Lakini sikujulikana uso
wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi
hapo kwanza, sasa anaihubiri Imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.139:1-3,13-14
1. Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.
(K) Uniongoze, Ee Bwana, katika njia ya milele.
2. Niende wapi nijiepushe na roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko;
Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. (K)
3. Ningezitwaa mbawa za asubuhi,
Na kukaa pande za mwisho za bahari;
Huko nako mkono wako utaniongoza,
Na mkono wako wa kuume utanishika. (K)
4. Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. (K)
SHANGILIO: Yn.14:5
Aleluya, aleluya!
Bwana anasema: mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima;
mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya!
INJILI:Lk.10:38-42
Yesu aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani
kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza
maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema,
Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie.
Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi;
lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu anataka watu wote watende mema kwa
moyo mnyofu, wapate kuokoka. Hivyo tuombe msaada
wake tukisema.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwatie moyo na ari ya uinjilishaji viongozi wetu wa
Kanisa, ili neno lako lipate kupenya mioyo ya watu
kwa wakati wake kokote waliko. Ee Bwana.
2. Uamshe ndani ya wote wenye mamlaka hapa duniani
roho ya uwajibikaji, na hivi kuwakumbusha watu
wao juu ya hasara ya uovu na faida ya kutenda mema.
Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote kulipatia neno lako nafasi ya kwanza
katika maisha yetu ya kila siku, tupate kukujua na kukutumikia
kwa ukarimu hasa katika nafsi za wenzetu
wenye shida. Ee Bwana.
4. Uwaamshie roho ya toba wote wanaoliudhi Kanisa
lako; kwani twaamini hata hao waweza kuongoka
wakawa wahubiri wazuri wa imani hiyo. Ee Bwana.
5. Uwarehemu waliokufani; na marehemu wetu wapewe
utukufu wa ufufuko wa Mwanao. Ee Bwana.
Ee Mungu, uliyetualika kulichagua fungu lililo jema na
lisiloondolewa kamwe, uyapokee maombi yetu. Kwanjia
ya Kristo Bwana wetu. Amina.