JUMANNE JUMA 28 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Gal.5:1-6
Somo katika waraka wa mtume Paulo kwa wagalatia. Katika ungwana huo kristo alituandikia huru kwa hiyo simameni wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa. Tazama mimi Paulo nawambia ninyi ya kwamba mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno. Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kutimiza torati yote. Mmetengwa na kristo mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. Maana sisi kwa roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya Imani. Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutotahiriwa , bali Imani itendayo kazi kwa upendo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:41,43-45,47-48(K)41
1. Ee bwana fadhili zako zinifikie na mimi
Naam wokovu wako sawasawa na ahadi yako
Nami nitamjibu neno anilaumuye
Kwa maana nalitumainia neno lako

(K) Ee bwana fadhili zako zinifikie na mimi.

2. Nami nitaitii milele na milele
Naam milele na milele
Nami nitakwenda panapo nafasi
Kwa kuwa nimejifunza mahusia yako (K)

3. Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako
Ambayo nimeyapenda
Na mikono yangu nitayainulia
Maagizo yako niliyoyapenda
Nami nitazitafakari amri zako. (K)

SHANGILIO: Zab.119:135
Aleluya, aleluya!
Umwangazie mtumishi wako uso wako, Na kunifundisha amri zako.
Aleluya!

INJILI: Lk.11:37-41
Yesu alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani. Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula. Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang’anyi na uovu. Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia? Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu zangu, kwa vile tunategemea ulinzi wa Mungu na malaika wake, tuombe.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Ili Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa waone fahari kukudhihirisha Wewe Mungu kwa maneno na matendo. Ee Bwana.

2. Wote waliopotea katika uzushi wajaliwe kurudi katika imani ya kweli, wapate kukutukuza na kuuabudu utukufu wako usio na uharibifu. Ee Bwana.

3. Sisi sote tujaliwe neema ya kutoionea aibu Injili, bali tujibidishe bila udhuru katika kukiri umungu Wako na uweza Wako wa milele. Ee Bwana.

4. Utuepushe na unafiki wa kifarisayo, ili imani yetu ionekane katika matendo ya upendo; na hivyo kutakaswa mwilini na rohoni. Ee Bwana.

5. Ndugu zetu waliofariki dunia wasamehewe dhambi zao na kuuona uso wako mtukufu huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetaka mwenye haki aishi kwa imani, utujalie hayo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.