JUMANNE JUMA 29 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Efe.2:12-22
Msisahau kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani. Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba. Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu. Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja. Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.85:9-14(K)9
1. Nisikie atakavyosema Bwana,
Maana atawaambia watu wake amani.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.

(K) Bwana anawaambia watu wake amani.

2. Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)

3. Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)

SHANGILIO: Yn.10:27
Aleluya, aleluya!
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya!

INJILI: Lk.12:35-38
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa kwa kutii kwake Bwana wetu Yesu Kristo ulimwengu umepata uzima, tumwombe Mungu kwa imani na matumaini.

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uzibariki juhudi za Maaskofu na Wachungaji wote wa Kanisa lako wanazozifanya, ili kutetea uhai na kuzilinda haki za binadamu na mali zao. Ee Bwana.

2. Serikali za mataifa yote zitende haki mintarafu uhuru wa kuabudu; na kuwa kiungo cha amani na uelewano kati ya dini au madhehebu yanayofarakana sababu ya ubinafsi. Ee Bwana.

3. Uwaingize watu wengi katika jamii ya wenye haki, ili nao wapate kutangaza msamaha wako ulimwenguni. Ee Bwana.

4. Kwa neema yako tustahimili kukesha mpaka ajapo Mwanao, Bwana wetu Yesu Kristo, kwa hukumu yake ya mwisho. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wanaomngoja Bwana wapewe uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu, twayaleta kwako maombi yetu haya. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.