JUMANNE JUMA 2 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: Isa.40:1–11
Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu, asema Mungu wenu. Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni
kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa, kwa kuwa amepokea kwa mkono wa Bwana
adhabu maradufu kwa dhambi zake zote. Sikiliza ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya Bwana,
nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu. Kila bonde litainuliwa, na kila mlima na kilima kitashushwa;
palipopotoka patakuwa pamenyoka, na palipoparuza patasawazishwa. Na utukufu wa Bwana utafunuliwa, na wote
wenye mwili watauona pamoja, kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya. Sikiliza, ni sauti ya mtu asemaye,
Lia! Nikasema, Nilie nini? Wote wenye mwili ni majani, na wema wake wote ni kama ua la kondeni. Majani yakauka,
ua lanyauka, kwa sababu pumzi ya Bwana yapita juu yake. Yakini watu hawa ni majani. Majani yakauka, ua lanyauka,
bali neno la Mungu wetu litasimama milele. Wewe uuhubiriye Sayuni habari njema, panda juu ya mlima mrefu;
wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema, paza sauti kwa nguvu. Paza sauti yako, usiogope; iambie miji ya Yuda,
Tazameni, Mungu wenu! Tazameni, thawabu yake I pamoja naye, na ijara yake I mbele zake. Atalilisha kundi lake
kama mchungaji, atawakusanya wanakondoo mikononi mwake; na kuwachukua kifuani mwake, nao wanyonyeshao
atawaongoza polepole.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.96:1–3, 10–13
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana likabirikini jina lake,
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku. (K)
(K) Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa.
2. Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake.
Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki,
Atawahukumu watu kwa adili. (K)
3. Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo.
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha. (K)
4. Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi,
Atahukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Siku ya Bwana i karibu, Tazama atakuja kutuokoa.
Aleluya.
INJILI: Mt.18:12–14
Siku ile, Yesu aliwaambia wafuasi wake. Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi
wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea? Hata akipata kumwona, amin, nawaambia,
amfurahia huyo zaidi, kuliko wale tisa na tisini wasiopotea. Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye
mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu anatualika kuwatuliza mioyo watu wake walio taabuni. Lakini hatuwezi kuifanya kazi hiyo peke
yetu. Tuombe msaada wa Mungu:
Kiitikio: Twakuomba utususikie.
1. Kwa kuwa sisi sote ni manabii, umjalie kila mmoja wetu kuhamasisha matengenezo ya njia atakayopita
Mwanao. Ee Bwana.
2. Sisi sote wenye mwili ni majani. Utuepushe na majanga yote yenye kunyausha na hata kukausha
mioyo yetu ikawa migumu. Ee Bwana.
3. Utuondolee woga wa aina yoyote, ili tuuhubiri ujio wa Mkombozi kwa sauti na nguvu; na watu wote
waielekeze mioyo yao kwako wewe uliye mchungaji wetu. Ee Bwana.
4. Uwapokee katika kundi la watakatifu wako ndugu zetu marehemu F. ili
asipotee hata mmoja. Ee Bwana.
Kungojea ujio wa pili wa Mkombozi wetu ni kujiandaa kwa siku ya mwisho wa maisha yetu hapa duniani. Kwa
kuwa hatujui Yesu Mchungaji wetu atakuja lini, utupe ushujaa wa kuyatawala maelekeo yetu mabaya ili atukute
tukikesha. Kwa huyo Kristo Bwana wetu. Amina.