JUMANNE JUMA 31 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Flp.2:5-11
Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo
alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana
nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;
tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti
ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;
ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya
nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.22:25-31(K)25
1. Nitaziondoa nadhiri zangu
Mbele yao wamchao.
Wapole watakula na kushiba,
Wamtafutao Bwana watamsifu;
Mioyo yenu na iishi milele.
(K) Kwako zinatoka sifa zangu, Ee Bwana.
2. Miisho yote ya dunia itakumbuka,
Na watu watamrejea Bwana;
Jamaa zote za mataifa watamsujudia.
Maana ufalme una Bwana,
Naye ndiye awatawalaye mataifa.
Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu. (K)
3. Wazao wake watamtumikia.
Zitasimuliwa habari za Bwana,
Kwa kizazi kitakachokuja,
Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake,
Ya kwamba ndiye aliyeyafanya. (K)
SHANGILIO: Mt.4:4
Aleluya, aleluya!
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Aleluya!
INJILI: Lk.14:15-24
Mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja na Yesu alimwambia, Heri yule atakayekula mkate
katika ufalme wa Mungu. Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akaalika watu wengi, akamtuma
mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa
tayari. Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti
niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda
kuwajaribu; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja. Yule
mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika,
akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya miji, ukawalete hapa
maskini, na vilema, na vipofu, na viwete. Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka,
na hata sasa ingaliko nafasi. Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani,
ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa. Maana nawaambia ya kwamba katika wale
walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Mungu ndiye mpaji wa neema na karama
mbalimbali. Tumwombe katika shida zetu:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Ili wote wanaoitwa kuihubiri Injili na kulihudumia
Kanisa lako wasitoe udhuru, bali waupokee wajibu
huo kwa moyo mkunjufu. Ee Bwanaa.
2. Ili wote wenye mamlaka serikalini wasione
madaraka kama ni kitu cha kushikamana nacho;
bali wawe watumishi wenye utayari hata wa kutoa
uhai wao kwa ajili ya wengine. Ee Bwana.
3. Ili ndugu, mali au kitu chochote tulichopewa hapa
duniani kitufae kwa wokovu; utuondolee vikwazo
kwa miito yetu. Ee Bwana.
4. Ili kila mmoja wetu atumie kipaji alichonacho kwa
manufaa ya wengine na kwa sifa na utukufu wako.
Ee Bwana.
5. Ili marehemu wetu wakaribishwe kwenye karamu ya
uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetupatia mahitaji yetu na kutuongoza
katika kweli yako, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.