JUMANNE JUMA 33 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO Ufu.3:1-6,14-22
Mimi Yohane, nilisikia Bwana anayeniambia: Kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa. Uwe mwenye kukesha, ukayaimarishe mambo yaliyosalia, yanayotaka kufa. Maana sikuona matendo yako kuwa yametimilika mbele za Mungu wangu. Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako. Lakini unayo majina machache katika Sardi, watu wasioyatia mavazi yao uchafu. Nao watakwenda pamoja nami hali wamevaa mavazi meupe, kwa kuwa wamestahili. Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri; na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako usionekane; na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu. Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.15:1-4(K)Ufu.3:21
1. Bwana, ni nani atakayekaa
Katika hema yako?
Ni mtu aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki.

(K) Yeye ashindaye, nitamketisha pamoja nami.

2. Asemaye kweli kwa moyo wake,
Asiyesingizia kwa ulimi wake.
Wala hakumtenda mwenziwe mabaya.
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao Bwana. (K)

3. Hakutoa fedha yake apate kula riba,
Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo hataondoshwa milele. (K)

SHANGILIO: Lk.8:15
Aleluya, aleluya!
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu, na kulishika.
Aleluya!

INJILI: Lk.19:1-10
Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake. Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona, walinung’unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

--------------

--------------
MAOMBI
Wapendwa, tunapaswa kuikiri imani yetu tuwapo katika mazingira yoyote na kwa gharama yoyote bila unafiki. Tuombe neema ya Mungu tukisema:-

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Viongozi wa Kanisa wazidi kuwahimiza watu wakutafute Wewe kwa gharama yoyote, wakukaribishe na kupata wokovu kwa imani yao kwako. Ee Bwana.

2. Uwasaidie viongozi wa serikali kusimamia vema raslimali za nchi yetu; ili utajiri uliopo uwanufaishe hasa wanyonge na wote wenye shida. Ee Bwana.

3. Wazazi wote wazidi kuwa mfano mzuri kwa jamii, wakidumu katika imani safi, mwendo wa adili katika kuzishika amri takatifu zilizotolewa nawe. Ee Bwana.

4. Sisi sote tudumu katika imani yetu bila unafiki, kwani hata tukiepukana na adhabu ya wanadamu sasa, hatutaweza kuepukana na mikono yako. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wasamehewe dhambi zao na kupokelewa kwako huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetafuta na kuokoa kile kilichopotea, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.