JUMANNE JUMA 34 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Ufu.14:14-19
Mimi, Yohane, niliona, na tazama, wingu jeupe, na juu ya wingu hilo ameketi mmoja, mfano wa Mwanadamu, mwenye taji ya dhahabu juu ya kichwa chake, na katika mkono wake mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa. Na yeye aliyeketi juu ya wingu akautupa mundu wake juu ya nchi, nchi ikavunwa. Kisha malaika mwingine akatoka katika lile hekalu lililoko mbinguni, yeye naye ana mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka katika ile madhabahu, yule mwenye mamlaka juu ya moto; naye akamlilia kwa sauti kuu yule mwenye mundu ule mkali, akisema, Tia mundu wako mkali, ukachume vichala vya mzabibu wa nchi, maana zabibu zake zimeiva sasa. Malaika yule akautupa mundu wake hata nchi, akauchuma mzabibu wa nchi, akazitupa zabibu katika shinikizo hilo kubwa la ghadhabu ya Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.96:10-13(K)13
1. Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike,
Atawahukumu watu kwa adili.
Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo.

(K) Bwana atauhukumu ulimwengu kwa haki.

2. Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)

SHANGILIO: Yak.1:21
Aleluya, aleluya!
Pokeeni kwa upole neno la Mungu, lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya!

INJILI: Lk.21:5-11
Watu wa kadha wa kadha walipokuwa wakiongea habari za hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe mazuri na sadaka za watu, Yesu alisema, Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Wakamwuliza wakisema, Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini ishara ya kuwa mambo hayo ya karibu kutukia? Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao. Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi. Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, sasa tupeleke maombi yetu kwa Mungu ambaye ni mpaji wa vyote tukisema.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwape nguvu na ari wahubiri wote wa neno lako, wapate kuwafundisha watu ukweli kuhusu maisha ya sasa na yanayofuata baada ya kifo. Ee Bwana.

2. Wafalme na watawala wote wajaliwe kuukiri uwepo wako, Wewe Mungu, Bwana wa mabwana, Mfalme wa wafalme, uliye na uwezo na nguvu na utukufu wote. Ee Bwana.

3. Utujalie sisi sote uliotuita kukutumikia kwa miito mbalimbali, kudumu katika imani uliyotujalia, tupate kuwavutia watu wengi kwako. Ee Bwana.

4. Utufunulie ishara zako za nyakati, tupate kuzisoma na kujiandaa vema kwa siku yako ya mavuno, mbele ya kiti chako cha huruma. Ee Bwana.

5. Ubatilishe mauti ya marehemu wetu na kuwajalia uzima usioharibika milele. Ee Bwana.

Ee Mungu, tumekuletea maombi yetu hayo tukiutumainia msaada wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.